Thursday 26 August 2010

BAADHI YA WAGOMBEA URAIS ZANZIBAR NGOMA NZITO.

Baadhi ya wagombea Urais Z'bar ngoma nzito



 Wahaha kutafuta wadhamini dakika za mwisho


 Wengine wasingizia Ramadhan inawakwamisha


 Dk. Shein avunja rekodi kwa watu wengi kujitokeza

Na Mwandishi wetu

WAKATI muda wa mwisho wa kurejesha fomu za kuwania Urais wa Zanzibar ukikaribia hapo Agosti 30, baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo wamekumbwa na wakati mgumu katika kutafuta wadhamini 200 kutoka kila mkoa Zanzibar, hali inayozua hofu huenda baadhi yao watashindwa kufanikisha kazi hiyo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini licha ya baadhi ya wagombea hao kuchukua fomu za urais mapema, hadi sasa wamekuwa katika harakati kubwa za kutafuta wadhamini hao katika mikoa ya Unguja na Pemba huku mafanikio yakiwa ni madogo.

Ukiachia mbali mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein na yule wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambao walifanikisha kazi hiyo kwa urahisi, wagombea wengine wote bado hawajakamilisha kazi hiyo, licha ya baadhi yao kusema kwamba wameshafikia hatua nzuri.

Dk. Shein ambaye anarejesha fomu yake Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) leo saa nane mchana, kwa kishindo alivunja rekodi ya kupata wadhamini wengi waliojitokeza kutaka kumdhamini kote Unguja na Pemba na baadhi ya wanachama kulazimika kukosa fursa hiyo.

Alipokuwa kisiwani Pemba juzi, Dk. Shein alipata makundi ya wanachama wa chama hicho na wananchi waliotaka kupata fursa ya kumdhamini, hatua iliyopelekea baadhi yao kukosa nafasi hiyo na kushauri idadi ya watu wanaotakiwa kuwadhamini wagombea iongozwe ili wengi zaidi waweze kupata fursa hiyo.

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia TADEA, Juma Ali Khatib alipozungumza na gazeti hili alisema kwamba alikuwa anaendelea na kazi hiyo ya kutafuta wadhamini katika mkoa wa Kaskazini Pemba na kwamba anatarajia kukamilisha kazi hiyo kabla ya muda wa mwisho.

Baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo walisema wamekuwa wakipata wakati mgumu kupata wadhamini hao kwa vile wananchi wengi hivi sasa hawapatikani kutokana na kuwepo katika harakati nyingi za mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

"Unajua wanachama wangu wengi ni wanawake ambao sasa wanakabiliwa na majukumu magumu majumbani kutokana na mwezi mtukufu wa Ramdhan", alisema mgombea mmoja wa Urais.

Mgombea wa Sauti ya Umma, Mussa Haji Kitole alisema kwamba alikuwa akiendelea vizuri na zoezi hilo katika mikoa ya Unguja kabla ya kuelekea Pemba kukamilisha wadhamini hao, ambapo amebakisha Mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Pemba.

Wanachama wa chama hicho, wameeleza kuwa hali hiyo inasababishwa na kuendelea kuwepo mgogoro ndani ya chama hicho, ulioanzia kipindi cha uchukuaji fomu ambapo chama hicho kiliwasilisha majina mawili ZEC, badala ya moja kama sheria inavyotaka.

Mjumbe wa Baraza Kuu la SAU, Peter Magwira, amesema suala la kupata wadhamini hawalielewi maendeleo yake, kwa vile Mgombea analisimamia mwenyewe na kueleza kuwa mgogoro wao watauwasilisha kwa Msajili wa Vyama Kisheria kwa hatua, baada ya kumalizika uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi hiyo kupitia NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis alisema kwamba tayari amepata wadhamini wanaohitajika na hivi sasa fomu zake zinahakikiwa tume ya uchaguzi Zanzibar.

Alisema tayari ameshakula kiapo mahakamani kutimiza masharti yaliyowekwa na ZEC, kwa wagombea wa nafasi ya Urais.

Naye Juma Ali Khatib ameeleza kuwa atarejesha fomu Jumatatu ijayo asubuhi, baada ya kukamilisha wadhamini kwa mujibu wa sheria, ambapo ataiarifu ZEC leo kuhusu mpango wake huo.

Jumla ya wagombea wanane wamechukua fomu za kuwania nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Wagombea hao ni Dk. Ali Mohammed Shein kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF, Juma Ali Khatib wa chama cha TADEA, Haji Ambar Khamis wa NCCR Mageuzi na Said Soud wa AFP.

Wagombea wengine ni Kassim Ali Bakar wa chama cha Jahazi Asilia na Haji Mussa Kitole wa Sauti ya Umma na Haji Khamis Haji wa chama cha NRA.





No comments:

Post a Comment