Tuesday, 17 August 2010

Rais Karume ashiriki Mkutano wa Wakuu wa SADC Namibia

Mafanikio, changamoto za nchi hizo zaelezwa

Rais wa Namibia awa Mwenyekiti mpya

Na Rajab Mkasaba, Namibia

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Amani Abeid Karume, ameshiriki katika sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa siku mbili wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika mji Mkuu wa Namibia, Windhoek.

Mkutano huo unafanyika chini ya Mwenyekiti mpya wa SADC, Hifikepunye Pohamba, Rais wa Namibia, miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika mkutano huo ni Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos, Rais wa Botswana, Luteni Jenerali Seretse Khama Ian Khama, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Congo, Joseph Kabila Kabange.

Wengine ni Rais wa Malawi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Profesa Bingu Wa Mutharika, Rais wa Msumbiji, Armando Emilio Guebuza, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Gedleyihleksa Zuma na viongozi wengineo.

Katika mkutano huo, Rais Karume amefuatana na mkewe Mama Shadya Karume, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, anayeshughulikia Fedha na Uchumi, Dkt Mwinyhaji Makame pamoja na viongozi na Maafisa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Rais Karume katika mkutano huo anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Mrisho Kikwete.

Mkutano huo, ulitanguliwa na Kikao cha Mawaziri kilichofanyika tarehe 14-15 Agosti mwaka huu, pamoja na Kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 11-13 Agosti mwaka huu, ambapo pia, Mkutano huo wa Wakuu wa nchi za SADC wa kila mwaka unaadhimisha miaka 30 ya kundwa kwa Jumuiya ya SADC.

Katika mkutano huo Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC kwa mwaka 2010/11 ambapo pia, mkutano huo utamchagua Makamo Mwenyekiti wa SADC.

Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohama, aliwakaribisha viongozi wote wa SADC na wajumbe pamoja na wageni walioalikwa katika mkutano huo wakiwemo wake wa Mais waliohudhuria na kueleza kuwa Namibia inajivunia mafanikio yaliopatikana katika Jumuiya hiyo na kusisitiza katika muda wake wa Uwenyekiti wa Jumuiya hiyo ataimarisha zaidi mafanikio yaliopatika.

Katika hotuba yake, Rais Pohamba alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika nchi za Jumuiya ya SADC na kuahidi kuyaimarisha zaidi ikiwa ni pamoja na umoja na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama.

Akito hotuba yake Mwenyekiti anaemaliza muda wake, Joseph Kabila, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, alieleza kuwa SADC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza programu zake mbalimbali ikiwemo kupiga vita umasikini, kupunguza vifo vya akina mama na watoto, usawa wa jinsia, kupiga vita maradhi, usalama sanjari na kuimarisha amani na utuli kwa maendeleo ya wananchi na mengineyo.

Rais Kabila alieleza kuwa suala zima la ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake hayo kati yake na viongozi wengine wa SADC limemuwezesha kufanya kazi zake akiwa Mwenyekiti wa SADC kwa ufanisi zaidi na kuzidisha mafaikio kwa Jumuiya hiyo.

Alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliopatikana pia, bado kuna changamoto zilizojitokeza katika mwaka 2009/2010, ambapo ana imani kuwa itaweza kufanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.

Akieleza juu ya mafanikio yaliopatikana katika nchi wanachama wa SADC, Rais Kabila alisema kuwa amani na utulivu miongoni mwa nchi hizo imezidi kuimarishwa na kuweza kupiga hatua kwa kiasi kikubwa.

Rais Kabila alisema kuwa uchumi na maendeleo kwa nchi wanachama umeweza kuimarika sambamba na kuendeleza programu za kupiga vita mradhi ya Ukimwi. Pia Rais Kabila alitoa pongezi kwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, kwa kufanikisha mashindano ya kombe la dunia yaliofanyika nchini mwake.

Aidha, katika mkutano huo Rais wa Zambia, Rupiah Bwezai Banda amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC kwa mwaka 2010/11.

Sambamba na hayo, katika mkutano huo wa Wakuu wa nchi wa Serikali wa SADC kutatolewa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa UNIVISA. UNIVISA ni mpango wa kuwa na viza moja kwa ajli ya watalii watakaotembelea nchi za SADC.

Utekelezaji wake ulitakiwa uanze kabla ya mashindano ya Kombe la Dunia yaliyofanyika mwezi Juni-Julai mwaka huu nchin Afrika Kusini.

Bado nchi wanachama zinafanya majadiliano kuhusu utekelezaji wake na hususan jinsi ya kugawana mapato yataokanayo na UNIVIS. Kwa sasa, nchi nne za Msumbiji, Namibia, Swaziland na Zimbwabwe zimejitoke kuanza majaribio ya utekelezaji wa UNIVISA.

Pamoja na hayo, katika uzinduzi huo washindi wa shindano la Waandishi wa habari na mashindano ya Insha walikabidhiwa zawadi zao ambapo kwa upande wa Tanzania mwanafunzi Cresensia Stephen kutoka skuli ya Sekondari Kifungiro aliyeshika nafasi ya tatu katika mashindano ya Insha ya shule za Sekondari alikabidhiwa zawadi yake na Rais Kabila.

Katika mkutano huo, viongozi mbali mbali wastaafu walihudhuria akiwemo kiongozi mwanzilishi wa Jumuiya hiyo Rais Kenneth Kaunda wa Zambia.

Katika sherehe hizo za ufunguzi, ngoma za utamaduni zilitumbuiza, Aidha, jana usiku kulitarajiwa kuwepo chakula maalum kilichoandaliwa na Rais mwenyeji wa mkutano huo, Rais Pohamba wa Namibia, ambacho na viongozi wakuu wa nchi na wageni wengine watashiriki.

No comments:

Post a Comment