Monday, 16 August 2010

Marekebisho ya 10 hayakuvunja Katiba ya Jamhuri- Wanasheria

Na Ramadhan Makame
MAREKEBISHO ya 10 ya katiba ya Zanzibar yaliyofanywa na kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichomalizika hivi karibuni hayakwenda kinyume wala kuvunja katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakizungumza na gazeti hili wanasheria mbali mbali waandamizi walisema hakuna kipengele cha katiba ya Jamhuri ya Muungano kilichoivunja kufuatia marekebisho hayo.

Walisema kufutwa kwa kifungu cha pili cha katiba ya Zanzibar kilichorekebishwa na kuandikwa upya kinachosomeka kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano ni jambo lililo wazi na ndivyo uhalisia lilivyo.

Wanasheria hao walisema Tanzania imeundwa na nchi mbili zilizo huru ambazo ni iliyokuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya watu wa Tanganyika, na hivyo kilichopotea ni utaifa wa Jamhuri hizo zilizoungana na si nchi.

"Kutokana kuwepo kwa Muungano huu Zanzibar na Tanganyika zimepoteza Utaifa na kubakia Utanzania lakini nchi ya Zanzibar bado ipo ndani ya Tanzania na hata kama Tanganyika wanataka iwepo hilo ni juu yao", alisema mmoja kati ya Wanasheria hao.

Walisema suala hilo sio geni kwani Marekani inaundwa na nchi 52 huku kila nchi ikiwa na sheria zake, mambo mengine ya kiutawala na kuiendeshaji lakini wanaunganishwa na taifa moja la Marekani.

"Kama mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yaliyofanywa yangeielezea hiyo nchi ya Zanzibar nje ya mipaka ya Tanzania hilo tungeliita uvunjwaji wa katiba ya Jamhuri vyenginevyo katiba haijavunjwa", alieleza.

Wakielezea kifungu 26(1) cha katiba ya Zanzibar kilichofutwa na kuandikwa upya kama kinavyosomeka kutakuwa na rais wa Zanzibar ambaye atakuwa mkuu wa nchi ya Zanzibar, Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, walisema kipengele hicho kimelenga kuainisha, kufafanua na kuweka wazi nchi itakayoongozwa na huyo Rais.

Walisema Zanzibar ina haki ya kutangaza mipaka yake na kufanya hivyo sio kosa ilimradi mipaka hiyo imo ndani ya taifa la Tanzania.

Wakizungumzia juu ya kufutwa na kuandikwa upya kifungu kinachompa mamlaka rais wa Zanzibar kugawa mikoa na wilaya bila ya ushauri wa Rais wa Jamhuri, walisema suala la Tawala za Mikoa si la Muungano.

"Tawala za mikoa si suala la Muungano, rais wa Zanzibar ana haki ya kuigawa Zanzibar kijiografia katika kuwaharakishia maendeleo wananchi wake vyovyote apendavyo bila ya kushauriana na rais wa Jamhuri kwani suala la Serikali za Mitaa si suala la Muungano au wanaolalamika watueleze".
 
Walisema marekebisho hayo yametafsiri kwa uwazi zaidi na kuondosha utata wa tafsiri ambao umekuwa ukitokea kila mara.

Vyombo vya habari vimeyavalia njuga kwa kuyalalamikia marekebisho hayo yaliyopitishwa Jumatatu iliyopita na Baraza la Wawakilishi huku vikisema katiba ya Jamhuri imekiukwa na Baraza la Wawakilishi kwa kufanya marekebisho hayo.

No comments:

Post a Comment