Thursday 19 August 2010

SHERIA MPYA HAIMKANDAMIZI MVUVI -- JUMBE

Sheria mpya haimkandamizi mvuvi - Jumbe



Na Raya Hamad, Melezo

MKURUGENZI Idara ya Uvuvi Mussa Aboud Jumbe, amesema sheria mpya ya Uvuvi iliyopitishwa na Baraza la Wawakilishi haina lengo la kuvikandamiza vipato wala kuwakomoa wavuvi.

Badala yake Mkurugenzi Jumbe alisema sheria hiyo namba 7 iliyotishwa na baraza hilo, imelenga kuweka nidhamu, matumizi mazuri na kulinda rasilimali za baharini kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Alisema wanaoihofia sheria mpya sambamba na kuipiga vita, ni wale wenye mitazamo ya matumizi mabaya ya rasilimali za baharini ambazo ni muhimu kimazingira na kiuchumi.

Mkurugenzi huyo alieleza hayo katika ukumbi wa hoteli ya Clove Inn kwenye mkutano uliozikutanisha kamati zote za wavuvi na mwani za kisiwani Pemba, ambapo alisema sheria hiyo ni nzuri mno kwa wavuvi wenye kujali maslahi ya baadae ya taifa hili.

Naye Mwanasheria wa Idara hiyo, Asha Mohammed Ahmeid, alisema sheria hiyo itasaidia kuondoa mgongano uliopo kwenye sheria ya awali ya mwaka namba 8 ya mwaka 1988.

Mwanasheria huyo aliwataka wavuvi waisome na kuielewa na sheria hiyo kwenye vifungu kadhaa kikiwemo kile kinachokataza wavuvi kuuza, kununua au kumiliki samaki waliovuliwa kwa njia za uvuvi haramu.

Alkisema katika kifungu hicho inakatazwa kabisa kununua, kuuza na hata kumiliki samaki waliovuliwa kwa vifaa vya uvuvi haramu kama vile bunduki, bomu, baruti, nyavu za macho madogo, utupa, juya na uvuvi wowote ambao haukubaliki kisheria.

Alisema sheria hiyo imetoa adhabu za kifungo, faini ama adhabu zote mbili, ambapo wavuvi wasio makini wataweza kukumbana na adhabu hizo.

No comments:

Post a Comment