Thursday 19 August 2010

AFISA WA PBZ AJINYONGA.

Afisa PBZ ajinyonga


Na Salum Vuai, Maelezo

MTU mmoja Othman Khamis Juma mkaazi wa Mombasa Unguja, amefariki baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba huko Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma Mohammed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema mwili wa marehemu huyo mwenye umri wa miaka 38, ulikutwa ukining'inia juu ya mshelisheli karibu na nyumba ya mama yake huko Kiembesamaki.

Alisema jeshi lake lilipata taarifa hizo jana asubuhi kati ya saa 12 na saa moja baada ya wapita njia kuuona mwili huo ukining'inia na kuiarifu afisi yake ambayo ilichukuwa hatua ya kutuma askari eneo la tukio.

Kamanda huyo alifahamisha kuwa, walipofika hapo askari hao walifanya taratibu zote za uchunguzi ikiwa pamoja na kupiga picha, kuufungua mwili huo na kuufikisha hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo, alisema bado haijafahamika kama marehemu alijinyonga mwenyewe au kuna watu wanaohusika na kitendo hicho.

Alisema uchunguzi uliofanywa haukubaini ujumbe wowote uliopatikana ndani ya mifuko ya nguo za marehemu unaoeleza sababu za kuchukua uamuzi huo, wala hakuna mtu aliyeweza kutoa ufafanuzi kama wanafahamu chochote juu ya nyendo za marehemu zisizokuwa za kawaida katika siku za hivi karibuni ambazo pengine zingeweza kuliongoza jeshi lake kujua chanzo cha kadhia hiyo.

Kamanda huyo alieleza kuwa, jeshi lake inalichukulia tukio hilo kuwa la kipolisi na linaendelea na uchunguzi zaidi.

Taarifa zilizopatikana na gazeti hili, zilieleza kuwa hadi anakutwa na masahibu huyo marehemu Othman Khamis Juma alikuwa mwajiriwa wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kitengo cha teknolojia ya habari (IT).

Baadhi ya watu wanaomfahamu marehemu, walisema hadi saa tisa usiku wa kuamkia jana, alionekana katika maeneo ya benki hiyo iliyopo Malindi mjini hapa kabla kuondoka na kuja kukutwa asubuhi ya jana akiwa ameshafariki.

Mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa jamaa zake ambapo mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo.

No comments:

Post a Comment