Na Fatma Kassim, Maelezo
BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi imegundua kuwepo dawa hatari endapo zitatumiwa na bindaamu.
Mrajis wa Bodi hiyo, Dk. Burhan Othman Simai alieleza hayo alipokuwa akitoa ripoti ya operesheni maalum iliyopewa jina la 'Operesheni Mamba III', ambayo iliendeshwa kwa kushirikiana jeshi la Polisi Tanzania na Shirika la Polisila Kimataifa Interpol.
Dk. Simai alisema katika operesheni hiyo, ilibainika kuwepo dawa zenye viwango duni na feki visiwani hapa ambazo nyingi zao hutengenezwa chini ya viwango kwa lengo la kujipatia kujipatia fedha za haraka.
Alisema Operesheni Mamba III, imegundua kuwepo aina ya dawa ya uzazi wa mpango iliyotengenezwa kwa miti shamba ambazo ina madhara makubwa endapo zitatumiwa na mwanamke.
Alisema iwapo mwanamke atatumia dawa hizo uzazi wa mpango ataongezeka uzito usio wa kawaida kutokwa na damu nyingi sambamba na mtoto atakayezaliwa na mama aliyetumia dawa hizo kupata ukubwa kabla ya kufikia muda.
"Dawa hii ya Kichina ya miti shamba ni hatari sana kwa mama na mtoto atakayezaliwa, akizaa wa mtoto wa kike atakua kabla ya siku zake na akiwa wa kiume takuwa na sauti nene kabla ya kufikia umri wa kubaleghe, pamoja na kuota nywele kwenye sehemu zao za siri kabla ya wakati ",alisema Dk. Simai.
Aidha katika ripoti hiyo, Mrajis huyo alianisha dawa nyengine feki zilizopatikana ni pamoja na dawa za kuongeza nguvu za kiume (urijali), chanjo feki ya pepo punda, dawa ya kutibia maleria na vipodozi vilivyopigwa marufuku.
"Madhara ya kutumia dawa bandia ni pamoja na kufeli kwa matibabu, usugu wa dawa na baadae hata kusababisha kifo", alisema Mrajis huyo.
Dk. Burhan alisema baada ya kuzikamata dawa hizo walizipima kwenye maabara yao pamoja na maabara ya Health science Authority ya nchini Singapore ambapo ilibainika kuwa hazifai.
Alisema tatizo la dawa duni na bandia ni ugaidi wa kibaologia na inaambatana na fedha chafu, uhalifu wa kifamasia, uhalifu wa hataza, uhalifu zidi ya ubinadamu na mauaji ya pole pole kwa ambae atatumia dawa zilizokuwa hazina viwango na zilizopita muda wa matumizi.
Alifahamisha kuwa takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kuhusiana na dawa feki na dawa bandia zinaonesha kuwa asilimia 10 ya dawa zilizo sokoni ulimwenguni ni bandia na feki na asilimia 25 dawa zipo katika soko la nchi masikini, na inakisiwa kuna watengenezaji wa dawa duni na bandia wanapata jumla ya dola bilioni 32.
Aliwataka wafanyabiashara kujali maisha ya watu na sio kufanya biashara tu kwa kujipatia fedha za haraka kwani athari kubwa itapatikana kufuatia dawa zilizopita muda, feki pamoja na vipodozi vyenye viambato vya sumu.
Operesheni hiyo ni ya kwanza na ya aina yake kufanyika Visiwani hapa ambapo ilifanyika sambamba kwenye nchi zote za Afrika Mashariki na ilifanyika Zanzibar nzima.
No comments:
Post a Comment