Monday 23 August 2010

Maelfu wajitokeza kumdhamini Dk.Shein


 Ambar akamilisha mikoa minne


 Juma Khatib mambo safi

Na Mwantanga Ame, ZJMMC


WANACHAMA wa CCM wamejitokeza kwa wingi kumdhamini mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, ili aweze kuwania kiti cha Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Katibu wa Idara ya Uenezi, Itikadi na siasa wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, aliyaeleza hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo Mjini Zanzibar kuhusu zoezi hilo linavyokwenda kwa pande wa mgombea huyo wa Urais.

Vuai alisema zoezi hilo linakwenda kwa kasi na kumejitokeza wanachama wengi wa kumdhamini Dk.Shein.

Dk. Shein alichukua fomu hiyo wiki iliyopita, huko Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo, ambapo baadhi ya wanachama wa CCM wa Mkoa wa Mjini walijitokeza kutaka kumdhamini.

Licha ya Mkoa huo, pia wanachama wengine ambao walijitokeza kutaka kumdhamini ni kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo zoezi hilo limepata mafanikio makubwa na linaendelea kisiwani Pemba.

Vuai alisema zoezi hilo lilitarajiwa kukamilka jana jioni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo hadi mchana wa jana wanachama wa chama hicho kisiwani Pemba walijitokeza kwa wingi kumdhamini mgombea huyo.

Hata hivyo, Vuai hakutaja idadi halisi ya wanachama waliojitokeza kutaka kumdhamini mgombea huyo ingawa alisema idadi yao ilipindukia kiwango kilichowekwa kisheria na Tume ya Uchaguzi cha watu watu 200 kwa kila Mkoa ambapo kila Mkoa waliowasajili walipindukia idadi hiyo.

"Watu wapo wengi sana wamejitokeza kumdhamini Dk. Shein, kwani kila Mkoa amepata watu kupindukia idadi ya Tume hatuna wasi wasi wa kupata wadhamini tumepata wa kutosha" alisema.

Akizungumzia juu ya tarehe ya kuanza kufanya kampeni zake kupitia chama cha Mapinduzi Zanzibar, alisema wanakusudia baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani visiwani Zanzibar.

Katibu huyo alisema kuwa licha ya Tume ya Uchaguzi kutangaza Agosti 10,2010 Chama cha Mapinduzi kinakusudia kuanza kufanya kampeni hizo mara tu baada ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

Alisema wameamua kufanya hivyo kwa lengo la kupisha mfungo huo umalizike ili kuwapa waumini wa dini ya kiislamu kuweza kukamilisha funga zao vizuri zaidi lakini hakusema tarehe kamili ya kuanza zoezi hilo.

Nae Mgombea Urais kwa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis, alisema amekamilisha Mikoa minne kupata wadhamini wake na hivi sasa yupo katika hatua za mwisho kukamilisha kazi hiyo katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema hadi sasa wadhamini waliojitokeza kumdhamini ni katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Kusini Pemba ambapo kazi ya mkoa uliobaki inatarajiwa kukamilika kuanzia kesho na kusema anatarajia kurejesha fomu Agosti 29, mwaka huu saa 8.00 za mchana.

Katibu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib, alisema amekamilisha kupata wadhamini katika mikoa yote a Unguja na hivi sasa yumo katika hatua za mwisho kudhaminiwa na wananchi wa kisiwa cha Pemba ambapo Mkoa mmoja tayari kazi hiyo imekamilika.

Kesho ameitaja kuwa siku atakayoweza utoa jibu la lini atarejesha fomu zake.









.

No comments:

Post a Comment