Wednesday, 18 August 2010

MACEMP YATUMIA 4B KUKAMILISHA UTEKELEZAJI WA MIRADI 251 ZANZIBAR.

MACEMP yatumia 4b/- kukamilisha utekelezaji miradi 251 Z'bar
Na Husna Mohammed (ZJMCC)

SHILINGI bilioni 4 zimetumika kukamilisha utekelezaji wa kuhifadhi mazingira ya bahari na ukanda wa pwani (MACEMP) kuanzia mwaka 2006 hadi sasa.

Fedha hizo zimetumika kwa miradi 251 ya jamii Unguja na Pemba, ikiwa ni miradi ya aina mbalimbali.

Meneja wa mradi wa MACEMP Zanzibar, Sheha Idrissa Hamdan, alisema kuwa hatua hio ni kubwa na kwamba imevuka lengo lililowekwa la miradi 160 kwa asilimia 156.

Alisema kwa upande wa Pemba jumla ya miradi 137 imetekelezwa yenye thamani ya shilingi 2,232,419,638 ambapo Unguja zimetumika shilingi 2,032,983, 080.35 kwa miradi 114.

Hata hivyo, alisema kuna miradi mipya 70 iliyoidhinishwa ambapo kila sehemu itakuwa ni 35.

Aliitaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni pamoja na uvuvi, ukulima wa mwani, uhifadhi wa rasilimali za magofu na mipango ya kihistoria, ufugaji wa kuku, shughuli za utalii na uhifadhi wa rasilimali za mikoko.

Miradi mingine ni pamoja na umwagiliaji maji, usanifu na utengenezaji kamba, ufugaji mbuzi, smaki, ujenzi wa masoko ya samaki, ufugaji wa makombe, upandaji miti, utengenezaji chumvi, ufugaji nyuki na na uhifadhi wa kasa.

Meneja huyo alisema pamoja na mambo mengine, miradi hiyo imewawezesha wavuvi kunyanyua hali zao za maisha.

Aidha lifahamisha kuwa mradi huo kwa kiasi kikubwa umeweza kuimarisha mazingira sehemu nyingi za ukanda wa pwani.

No comments:

Post a Comment