Monday 23 August 2010

MAREKANI YAPONGEZA ZANZIBAR KWA KUPEVUKA KIDEMOKRASIA

Marekani yaipongeza Zanzibar kwa kupevuka kidemokrasia

 Ali Mzee avipongeza vyombo vya habari kufanikisha kura ya maoni


Na Mwandishi wetu


SERIKALI ya Marekani imeipongeza Zanzibar kwa kuonesha kukomaa kidemokrasia, na kuamua kujenga Zanzibar mpya kufuatia kupiga kura ya maoni ya muundo mpya wa kisiasa kwa amani na utulivu Julai 31 mwaka huu.

Pongezi hizo zimetolewa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt, alipozungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Ali Mzee Ali, Afisi za Baraza hilo Mbweni Zanzibar jana.

"Nilipofika Zanzibar kwa mara ya kwanza, nilieleza hamu na matumaini yangu kwamba wananchi wa visiwa hivi vizuri wataungana na kujenga Zanzibar mpya iliyojaa amani.......nashukuru ndoto yangu hiyo imetimia muda mfupi sana" alisema Balozi huyo.

Balozi Lenhardt alieleza hatua hiyo ya viongozi na wananchi wa Zanzibar, imejenga historia ulimwenguni kote na kuichora Zanzibar katika ramani ya nchi zinazofuata demokrasia ya kweli.

Akizungumzia jengo jipya la Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Balozi Lenhardt alisema ni kiashirio kikubwa kwamba Wazanzibari wameamua kubadilika na kujenga Zanzibar mpya yenye mambo mapya ya kimaendeleo.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, Balozi huyo alisema una kila ishara ya kuwa wa mafanikio, huru na uliojaa amani, kama ilivyokwishaonekana kupevuka kwa wananchi wa Zanzibar, walipopiga kura ya maoni mwezi uliopita.

Alisema ni jambo la kufurahisha kuona Wazanzibari ndiyo wenye kufanya maamuzi kuhusiana na mustakbala wa nchi yao, pamoja na kushirikiana kuendesha nchi kwa pamoja baada ya uchaguzi mkuu na kuzifanya sauti za wananchi wote kusikilizwa, jambo ambalo Marekani na dunia nzima inalipongeza.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya watu sita ya Baraza la Wawakilishi iliyoundwa kusimamia kura ya maoni, Ali Mzee Ali, aliishukuru Serikali ya Marekani kwa kuunga mkono harakati za maendeleo na kujenga amani na utulivu Zanzibar, ikiwemo kuendeshwa kura ya maoni Julai 31 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alimuomba Balozi huyo kuwasilisha salamu za shukurani kutoka kwa wananchi wa Zanzibar kwa Rais Barack Obama wa Marekani, kutokana na hatua za nchi hiyo kuiunga mkono Zanzibar katika kujenga taifa lenye amani na utulivu wa kudumu.

Mzee ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, aliwapongeza waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali nchini, kwa kutoa mchango mkubwa kwa Kamati hiyo, ambao ulisaidia kutoa taaluma kwa wananchi wa Unguja na Pemba kuhusiana na kura ya maoni.

Alisema bila ushiriki kikamilifu wa wanahabari, basi kazi ya kamati yake kuelimisha wananchi kuhusiana na kura ya maoni ingekuwa ngumu, ikizingatiwa muda uliokuwepo ulikuwa mfupi.

Aliwataka waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi zao kwa uzalendo na kuelimisha wananchi kuhusiana na mambo yatayojenga mustakbala mzuri kwa nchi yao.

Akizungumzia umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru, Balozi Lenhardt, alisema vina mchango mkubwa ndiyo maana vikafanikisha kura ya maoni kuhusiana na muundo mpya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuvitaka mara zote kuwa tayari kuonesha changamoto zinazoikabili jamii ili ziweze kurekebishwa.

No comments:

Post a Comment