Saturday, 21 August 2010

NEC YAZIBWAGA PINGAMIZI

NEC yazibwaga pingamizi


Na Mwajuma Juma

TUME ya Uchaguzi ya Taifa ya Tanzania (NEC), Wilaya ya Mjini imezitupilia mbali pingamizi dhidi ya wagombea wa tatu wa nafasi za Ubunge.

Tume hiyo ilipokea pingamizi dhidi ya wagombea wa Ubunge wa majimbo Kikwajuni na Mpendae baada ya wagombe hao kwenda kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na tume hiyo.

Akizungumza na gazeti hili Msimamizi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Masha Said, alisema Yussuf Masauni anayewania Ubunge jimbo la Kikwajuni aliekewa pingamizi na mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya CUF Dk. Idarous Habib Mohammed.

Katika madai yake mgombe huyo wa CUF liwasilisha tuhuma za Masauni kughushi umri kwenye fomu yake ambapo alidai amezaliwa Oktoba 3, mwaka 1979 wakati fomu ya kuwania Ubunge alijaza kazaliwa Oktoba 3, mwaka 1973.

Kwa upande wa mgombea wa jimbo la Mpendae mgombea Ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM Salim Hassan Turkey aliwekewa pingamizi na wagombea wawili.

Turkey aliwekewa pingamizi Hussein Hassan Sultani ‘Malayka’ mgombea wa nafasi hiyo kwa tiketi ya Jahazi Asilia na Mohammed Hemed wa CHADEMA.

Katika dai lake dai lake la msingi Hussein Hassan Sultani ‘Malayka’ alisema Turkey ametoa rushwa huku mgombea wa CHADEMA Mohammed Hemed akidai Tukery amekiuka sheria ya gharama za uchaguzi.

“Malayka katika pingamizi yake hiyo alidai kuwa Turkey alitoa rushwa ya shilingi 200 kwa kila aliyekuwepo katika Tawi la CCM la Mpendae pamoja na mchele”, alisema msimamizi huyo.

Hata hivyo Msimamizi huyo wa NEC, alisema kwamba katika pingamizi hizo zote tatu hakuna hata mlalanmikaji alietoa kielelezo cha kuthibitika makosa na badala yake Tume imeamuwa kuwathitisha wagombea wote wawili na kwamba ni halali.

“Hakuna vielelezo vyovyote vya kuthibitisha hilo, ambapo kwa upande wa mlalamikaji Malayka alileta mashahidi watatu ambao wote hawajathibitisha kutolewa kwa rushwa bali kila mmoja alisema kwamba Turkey alitoa sadaka”, alisisitiza Masha na kuongeza kwamba kwa msingi huo nimewateua rasmi kuwa wagombea halali kupitia chama cha Mapinduzi (CCM).

Katika hatua nyengine mgombea wa CUF Dk. Idarous yeye ameamua kukata rufaa Tume ya Uchaguzi ya Taifa baada ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa na tume ya Wilaya ya mjini.

Katika rufaa yake hiyo ambayo aliiwasilisha majira ya saa 7:00 mchana mlalamikaji huyo alidai kuwa katika usikilizwaji wa pingamizi yake hakutendewa haki ikiwemo kutoitwa yeye wala mlalamikiwa katika usikilizwaji huo, dai ambalo msimamizi wa Tume hiyo alilipinga.

Msimamizi huyo alieleza kuwa mlalamikaji huyo wa CUF katika rufaa yake alitoa taarifa za uongo kutokana na kuwa wakati wa kusikiliza pingamizi hizo waliwaita kwa pamoja na kila mmoja alitoa maelezo yake.

“Nashangaa baada ya kupata rufaa hii kuona mlalamikaji anasema hakutendewa haki, wakati niliwaita wote wawili na kila mmoja alitoa maelezo yake”, alisema.

Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya wilaya ya Mjini imetoa fomu kwa wagombe 65 wanaowania kuteuliwa nafasi ya Ubunge wa ambapo wagombea 55 ndio waliorejesha fomu hizo.

No comments:

Post a Comment