Tuesday 17 August 2010

MSICHANA WA MIAKA 16 AONDOKA NA 500,000/= MASHINDANO YA QURANI

Msichana miaka 16 aondoka na 500,000/- mashindano ya Qurani


Na Aboud Mahmoud

MASHINDANO ya kuhifadhi kuran kimataifa yameanza rasmi visiwani Zanzibar jana katika sehemu za Masjid Noor Muhammad kwa Mchina ambayo yalikuwa kwa upande wa wanaume na kwa wanawake yalifanyika katika ukumbi wa skuli ya Haile Sselassie.

Katika mashindano hayo ambayo yameshirikisha juzuu 10,20 na 30 na kuwashirikisha wanafunzi kutoka Mikoa ya Zanzibar, Dar es Salaam,Tanga na Singida yalionekana kuvutia waislamu wengi ambao wameshiriki katika mashindano hayo.

Mwanafunzi Amina Ali Soud kutoka Zanzibar mwenye umri wa miaka 16 alikuwa mshindi wa ufunguzi wa mashindano hayo kwa juzuu 30 ambapo alipata alama 96 na kuzawadiwa fedha taslim shilingi 500,000,Kanga, Sketi na Blauz.

Aidha, mshindi wa pili alikuwa ni Tawhida Salum Said kutoka Zanzibar aliepata alama 94 na kuzawadiwa shilingi 400,000,Kanga na Kitambaa ambapo mshindi wa tatu Asya Mohammed Salum kutoka Zanzibar aliepata alama 88 na kupata zawadi ya shilingi 300,000 Kanga na Blauz.

Kwa upande wa washiriki wa juzuu 20, mwanafunzi Mize Abdullah Fakih, (14) alifanikiwa kuondoka na ushindi baada ya kupata alama 94 na kukabidhiwa zawadi ya shilingi 230,000 Kitambaa na Kanga.

Mshindi wa pili alikuwa ni Mkiwa Mussa Aziz aliepata alama 93.5 na kuzawadiwa shilingi 180,000 taslim, Kanga na Blauz ,wakati mshindi wa tatu alikuwa ni Suria Ali Bakar, kutoka Dar es Salaam aliepata alama 93 na kupata zawadi ya shilingi 130,000 taslim Kanga na Mtandio.

Aidha, kwa upande wa juzuu moja mshindi alikuwa ni Salha Faki Khatib kutoka Zanzibar aliepata alama 100 na kupata zawadi ya fedha taslim 130,000 Kanga na Msahafu,huku mshindi wa pili alikuwa ni Safia Nassor Omar (12) aliepata alama 96 na kupata fedha taslim shilingi 100,000 Kanga na Msahafu.

Nae mshindi wa tatu alikuwa ni Salma Fadhil Ali aliepata alama 94.5 na kupata zawadi ya shilingi 80,000 Kanga na Msahafu.

Mashindano hayo ambayo yalionekana kuvutia wanawake wengi wa kiilslamu visiwani Zanzibar yanatarajiwa kuendelea leo katika ukumbi huo huo wa Haile Selassie kwa kushindanisha juzuu kuanzia 5,15 na 25.

Nae Mwantanga Ame (ZJMMC), anaripoti kuwa waislamu nchini wameshauriwa kuona umuhimu wa kuwekeza kwa kuanzisha skuli za kiislamu ili kuwafanya watoto wa kiislamu kuzidi kuwa na elimu bora na kufuata maadili mema ya kiislam.

Ushauri huo umetolewa na Sheikh Suweid Ali Suweid wakati akitoa nasaha zake katika mashindano ya kuhifadhi kur-ani, kwa wanaume yaliofanyika masjid Noor Muhammad (SAW) Mjini Zanzibar.

Mashindano hayo yaliwashirikisha wanafunzi wa madrasa mbali mbali za Unguja, Pemba, Kenya na Rwanda.Tanzania Bara, Uganda, Burundi, Comoro, Zambia na Msumbuji.

Sheikh huyo alisema ni lazima kwa waumini wa dini ya kiislamu kuona umuhimu wa kuwekeza kwa kuanzisha skuli za kiislamu ili kuweza kukuza viwango vya elimu kwa waumini wa dini hiyo ipo chini na idadi ya waislamu wanaopata elimu ya juu bado ni ndogo.

Alisema hali hiyo inajitokeza kutokana na wengi wa waislamu kuacha kuwekeza eneo hilo ambapo skuli za aina hiyo kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar bado idadi yake ni ndogo hadi vyuo vikuu.

Akitoa mfano alisema kwa Tanzania hadi hivi sasa kuna chuo kikuu kimoja cha kiislamu wakati katika baadhi ya nchi zikiwemo za Afrika Mashariki zimekuwa na idadi kubwa za vyuo vikuu vya kiislamu pamoja na skuli.

Sheikh Suweid, alisema ili kuweza kuiga hilo ni lazima kwa waislamu wenye uwezo wajikubalishe kuanzisha skuli za kiislamu katika ngazi tofauti ikiwemo ya msingi sekondari hadi vyuo vikuu.

"Waislamu hawajaamka kwa kuanzisha skuli zao kuna nchi zina skuli nyingi zinazotowa elimu kwa waislamu na Tanzania mpaka sasa tuna chuo kimoja tuu lazima tuwekeze huku kwani kuna mabadiliko ya kidunia yanakuja msukumo wetu bado ni mdogo sana" alisema Suweid.

Alisema ni lazima hilo walieangalie kwa kutambua hivi sasa wanaingia katika zama za badiliko ya elimu katika dunia kwa vile ni muhimu kwa kujenga misingi madhubuti ya maisha ya mwanadamu kwani hawataweza kufanya jambo lolote ama kwenda popote bila ya kuwa na elimu.

Akiendelea alisema,inasikitisha kuona uduni huo haupo katika ukosefu wa skuli zaKiislamu pekee na umekuwa ukizikumba hata madrasa ziliopo kutokuwa na viwango vya kisasa katika mazingira ya kutoa elimu kwa watoto wa kiislamu.

Akitoa mfano alisema nyingi ya madrasa hasa za vijijini hivi sasa zimekuwa zikionekana kuwa katika mazingira mabaya yasioridhisha matumizi yake kiafya kwa kutumia vyumba vidogo ama mabada huku idadi ya wanafunzi hufikia hadi watoto 120.

Alisema hali hiyo inaweza kuwasababishia wanafunzi kupata matatizo kwani hawako katika usalama wakiafya kutokana na mazingira ya kubanana wakiwa madarasani.

"Inasikitisha waisalamu tunapiga kelele watoto skuli wanakaa chini lakini tunasahau na katika madrasa zetu watoto wanatakiwa nao wakae katika madeski sasa tuzifanyeni madras zetu ziwe za kisasa sio kupigia kelele skuli tuu"

Alisema ikiwa waisalamu watashriki kutoa michango yao ni wazi eneo la madrasa litaeza kuwa namabadiliko kielimu pamoja nakustawisha jamii kuwa katika maadili mema kwani wengi wa waislamu wamekuwa wakitoa michango yao katika mambo mbali mbali lakini upande huo wameusahau.

"Tuangalie wapo watu hivi sasa waislamu wanasomesha watoto wao nje wanatumia fedha nyingi sana kama fedha hizi zingekuwa zimechangiwa kuwekeza skuli hizi hapa Zanzibar tungekuwa mbali na waislamu wengi wangepata fursa za kusoma humo" Alisema Sheikh Suweid.

Akitoa mfano alisema inasikitisha kuona hivi sasa baadhi ya Wazee kuwa wakali pale wanapodaiwa michango ya madrasa huku wakisahau muda na kazi hiyo anayojipa mwalimu kumsomesha mtoto wake huku akiwa mwepesi kulipia ada za skuli.

Alisema ni vyema kwa wazazi kuiangalia kasoro yao hiyo kwa kuhakikisha wanaotoa michango yao bila mivutano ili kukuza elimu za watoto wao.

Alisema leo hii inapendeza kuona vijana wengi wameamua kujitokeza kushiriki katika mashindano ya Kur-ani, idadi ambayo ni ya kupongezwa kutokana na mchango uliotolewa na walimu ambapo wazazi wanahitaji kuuthamini kwa kuhakikisha wanalipa ada kwa wakati.

Aidha, Sheikh huyo, aliwataka Wazazi kuhakikisha wanafuatilia nyendo za watoto wao wakiwa masomoni ili kuona maendeleo yao yanaenda vipi kwani jambo hilo limekuwa likisahaulika.

Alisema hilo linajitokeza hata pale watoto hao wanapotaka kushiriki katika mashindano makubwa lakini hakuna hata mzazi wake mmoja anaejitokeza kumuunga mkono mtoto huyo.

Alisema ni vyema kwa waumini wa dini ya kiislamu kuona wanaachana na tabia hiyo na badala yake wanashirikiana pamoja na walimu katika kufuatilia nyendo za watoto wao.

Nae Mkuu wa Jumuiya ya Kuihifadhi Kur-ani Suleima Omar Baramia, akitoa nasaha zake alisema mashindano ya uhifadhi yamekuwa yakikua siku hadi siku jambo ambalo litahitaji kupata mchango mkubwa kutoka kwa waislamu ili kuyafanya kuwa na hadhi zaidi.

Katika mashindano hayo wanafunzi wa kizanzibari walifanikiwa kuchukua nafasi za kwanza hadi ya tatu na kupata zawadi za fedha taslim.

Mkuu wa Majaji katika mashindano hayo Masoud Abubakar Gulam alisema walioshika nafasi za kwanza kwa waliohifadhi juzuu ya tano kati ya washiriki 10 ni Abdulsalami Juma Khamis (10), wa Zanzibar aliepata zawadi ya shili 100.000, Mohammed Aboud Mohammed (Zanzibar) aliongoza kwa asilimia (99.5) na kupata shilingi 80,000, na Ali Shaame (Zanzibar) aliepata zawadi ya shilingi 70,000 ambapo washiriki wengine walipata zawadi ya shilingi 40,000.

Mkiendelea alisema upande wa juzuu 15 alieshika namba moja ni Abdalla Mohammed Abdalla (15) (Zanzibar) alipata asilinia 97 na kufanikiwa kunyakuwa kitita cha shilingi 160,000, Yassin Masoud Mohammed, (Zanzibar) Alieshinda kwa asilimia 94.5 na kuchukua zawadi ya shilingi 130,000 na Ibrahim Khamis Omar (Zanzibar) alishika nafasi ya tatu na kupata zawadi ya shilingi 100.000.

Msimizi huyo alisema  upande wa juzuu 25, alieshika namba moja ni Khamis Ali Khamis (Zanzibar)aliepata asilimia 98.5 ambaye alizawadia shilingi 200.000, Omar Ali (Zanzibar) aliepata 180,000 na Abdulrahman Ramadhan Abdulrahman, kutoka Dodoma, alieshika nafasi ya tatu na kupata zawadi ya shilingi 180,000

No comments:

Post a Comment