Monday, 30 August 2010

WAGOMBEA WARUDISHA FOMU KWA MBWEMBWE.

Wagombea warudisha fomu kwa mbwembwe



 Wengine wathibitisha kukubali matokeo

Na Mwantanga Ame, ZJMMC

WAKATI zoezi la urejeshaji fomu za kuwania nafasi ya Urais wa Zanzibar, Uwakilishi na Udiwani, likikamilika baadhi ya wagombea wamefanikiwa kurejesha fomu zao huku wengine wakiwa wamekwama baada ya kuzuka mivutano ndani ya vyama vyao.

Zanzibar Leo, jana asubuhi imeshuhudia baadhi ya wagombea wa vyama vilivyochukua fomu kuwania nafasi hizo wakizirejesha Tume ya Uchaguzi Zanzibar pamoja na Afisi ya Tume Wilaya ya Mjini.

Mgombea wa kwanza ambaye alijitokeza katika Tume hiyo majira ya saa 4.20, ni wa Chama cha TADEA, kilichowakilishwa na Katibu wa Chama hicho upande wa Zanzibar Juma Ali Khatib, na kufuatiwa wa Chama cha Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wenyeviwanda na Wakulima, Said Soud na baadae ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi Zanzibar Haji Ambar Khamis.

Wagombea hao walifika Tume hiyo wakiwa katika mbwembwe za kusindikizwa na wapambe wao kwa misururu ya magari yaliyokuwa yakipiga honi barabarani huku wakiongozwa na kasida za dufu pamoja na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kauli mbiu za vyama vyao.

Wagombea hao walikabidhi fomu hizo kwa Mwenyekiti wa Tume hiyo Khatib Mwinchande na kuiarifu Tume hiyo kuwa wamekamilisha kupata wadhamini kwa idadi waliyotakiwa ya wadhamini 200 kwa kila Mkoa wa Zanzibar.

Akizungumza baada ya kupokea fomu hizo Mwenyekiti wa Tume hiyo, alivitaka vyama vyote kuhakikisha vinajiandaa vyema kuingia katika uchaguzi wakidumisha hali ya amani na utulivu kwa kufanya kampeni za kistaarabu.

Alisema haitategemewa baada ya wagombea hao kupitishwa na Tume hiyo kuwa wagombea halali wa uchaguzi ujao, na vyama hivyo kuendesha kampeni kwa kutoa matusi hadharani .

Mwenyekiti huyo alisema Zanzibar hivi sasa haihitaji kampeni chafu na ndio maana Tume yake imeamua kutoa uhuru wa kutosha wa kuvipa fomu kwa kila chama ikiwa na lengo la kukuza demokrasia hapa nchini.

Alifahamisha kuwa demokrasia inayohitajika kufuatwa ni ya kuwaelezea watu juu ya maendeleo gani vyama vyao vinakusudia kuwapatia wananchi na sio demokrasia ya kupigana.

"Tushindane lakini tusipigane", alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliwataka wagombea hao kuwasilisha ratiba zao za kampeni ili Tume hiyo iweze kuandaa ratiba ya kampeni ya Kitaifa.

Wakitoa shukrani zao vyama kwa nyakati tafauti wagombea hao walieleza kuwa watahakikisha wanatimiza masharti ya Tume hiyo kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuipongeza Tume hiyo kwa kuwapa haki sawa vyama vyote.

Mgombea wa Chama cha TADEA Juma Ali Khatib, alisema Chama chake baada ya kupata ridhaa ya wananchi kipaumbele chao ni kuhakikisha nafasi za viti vya wanawake inafikia asilimia 50 wakiwa na lengo la kuwawezesha kushika uongozi katika mambo mbali mbali.

Aidha, Mgombea huyo alisema suala jengine ambalo atalishughulikia ni kuimarisha elimu kwa wanafunzi wa Zanzibar, ili wasome vizuri kwa lengo la kuwawezesha kukabiliana na ajira katika soko la Afrika Mashariki.

Nae Mgombea wa Chama cha Wakulima na Wenyeviwanda (AFP), Said Soud, alisema chama chao kitakuwa na vipaumbele vinne kikiwemo cha kukuza kilimo na biashara kwa kila Mkulima kupandiwa na mazao ya asili bure kazi ambayo itasimamiwa na serikali.

Alisema Wananchi katika kuitekeleza sera hiyo kila mtu ataweza kupandiwa miti ya minazi bure katika shamba lake na maeneo ya wazi huku akipata ofa ya kulimiwa katika shamba lake mara moja kwa mwaka kazi ambayo itafanywa kwa kutumia matrekta ya serikali.

Eneo jengine ambalo alilitaja ni linalohusu elimu ya juu kufanywa kuwa ni la Zanzibar, badala ya kuwa chini ya usimamizi wa Tanzania bara huku, na pia kujenga Chuo Kikuu Pemba badala ya Unguja pekee na kukuza sekta ya afya kwa kupata wataalamu zaidi.

Nae Mgombe wa Chama cha NCCR Mageuzi, Haji Ambar Khamis, alisema Chama chake kitakubali matokeo yoyote yatayojitokea katika uchaguzi ujao kwa vile wanaamini kuwa Tume hiyo itawatendea haki vyama vyote.

Makamu huyo alisema Chama chao kitahakikisha kinadumisha amani na utulivu kwa wakati wote wa kampeni zao kwani kimepata msukumo mzuri wa kuwania nafasi hiyo kwa vile mazingira yaliyopo hivi sasa ni tofauti na uchaguzi wa mwaka 2005.

Wagombea hao wote waliikabidhi Tume ya Uchaguzi shilingi milioni 2 ikiwa ni ada ya uchukuaji wa fomu hizo kwa kila Mgombea anaewania nafasi hiyo

Afisa Msimamizi wa Wilaya ya Mjini Mwanapili alifahamisha kuwa katika majimbo 10 ya Wilaya hiyo wagombea 20 wa CCM na CUF, wameresha fomu hizo huku wagombea 10 kutoka chama cha NCCR Mageuzi, Tadea, Jahazi, NRA baadhi yao yao wameshindwa kurejesha fomu hizo.

Alisema wagombea wa Udiwani 57 waliochukua fomu walirejesha fomu zao na pingamizi kwa wagombea hao zinatarajiwa kuanza kuwekwa Septemba 2 hadi 3 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment