Tuesday, 17 August 2010

DK. SHEIN NIMEJIANDAA KUOBGOZA SERIKALI KWA UFANISI MKUBWA.

Dk. Shein: Nimejiandaa kuongoza Serikali kwa ufanisi mkubwa

Asema hatawavumilia viongozi wazembe
Asema hakulelewa kudharau, kuchukia, wala kubagua watu



Na Mwanajuma Abdi

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein amesema amejiandaa kuongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ufanisi mkubwa na kamwe hatowavumilia watendaji wataoweka mbele ubinafsi.

Dk. Shein, ambae ni Makamo wa Rais wa Tanzania, alisema yeye sio mkimya wala "regerege" kama wanavyomfikiria baadhi ya watu, lakini ni mtendaji wa kazi kwa vitendo na mara nyengine yakizidi husema, hivyo aliwatahadharisha viongozi wataokiuka maadili na kufanya kazi kwa mapenzi na maslahi yao binafsi, ambapo alisisitiza wawaulize, Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano Tanzania aliofanya kazi nao.

Kauli hiyo aliitoa jana, alipowahutubia wagombea waliopita katika kura ya maoni ya CCM, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani, Wastaafu wa majimbo na wanaCCM, katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

"Sitoruhusu kiongozi katika Serikali yangu kufanya kazi kwa mapenzi yake binafsi wala bakabaka, ninawajua watu na mimi wananijua kama sipendi kusema na mtu anapokuwa anasema maneno makali wakati mwengine huguna tu lakini ni mtendaji zaidi", alisisitiza Dk. Shein.

Alifahamisha kuwa, kila zama na viongozi wake, ambapo hata vitabu vinne vya Mwenyezi Mungu vya kupigania dini yake cha Taurati Nabii Mussa, Zabur alikabidhiwa Nabii Daud, Injil- Nabii Issa na Quran Mtume Muhammad (S.W.A), hivyo yeye atakuwa wa awamu ya saba lakini lengo ni moja katika kuendeleza kukitumikia Chama cha Mapinduzi na kuenzi Mapinduzi ya Zanzibar, kudumisha Muungano wa Tanzania na kuzidisha umoja, mshikamano pamoja na kuimarisha amani na utulivu nchini.

Dk. Shein ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, aliwaeleza wanaCCM hao kwamba hakulelewa katika misingi ya kudharau watu, kuchukia wala kubagua na kusema kama kuna mtu katika ukumbi huo aliyemfanyia kati ya mambo hayo ajitokeze.

Aliwakumbusha wanachama kuwa yeye ni mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa CCM, ambapo kwa mwaka huu wagombea 837 akiwemo yeye walijitokeza kugombania nafasi za Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani vikiwemo viti maalum kwa Zanzibar, hivyo ataungana nao kama makamanda wa kukipatia ushindi wa lazima chama hicho kama inavyoeleza katika ibara ya 5 ya Katiba ya CCM katika kushika dola ya nchi.

"Katiba ya CCM ibara ya 5 kifungu cha kwanza kimesema ushindi katika uchaguzi wa Serikali kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ni lazima kwa Chama hicho katika kuongoza Dola", alifafanua Dk. Shein.

Alisema nyenzo za CCM za ushindi zipo wazi kwani kina heshima kubwa katika nchi, sambamba na kuwa na historia ya kuwatetea watu na kuondosha ubaguzi pamoja na kutekeleza kwa vitendo ilani na sera zake katika kuwaletea maendeleo, ambapo msingi huo wa mafanikio hayo umetokana na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na viongozi waliomfuata hadi sasa.

Akigusia uchumi wa Zanzibar, alisema unakuwa siku hadi siku kwa kasi kubwa, ambapo ifikapo Dira ya Maendeleo ya 2020 unatakiwa ufikie zaidi ya asilimia nane ili wananchi wake waweze kuishi katika maisha ya kati na kati, kuwaondoa kwenye umasikini.

Alisema uchumi huo unakua kutokana na ushirikiano na kufanyakazi kwa juhudi zaidi, ambapo alitao mfano nchi kama Uingereza uchumi wake unakua kwa asilimia mbili na Urusi asilimia tatu.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Ferouz wakati akimkaribisha Dk. Shein alisema idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu, inaonesha wazi kwamba CCM kina makada wengi na wenye sifa za kuongoza katika vyombo vya dola.

Alifafanua kuwa, idadi hiyo pia inaonesha ushindi wa Chama hicho katika uchaguzi mkuu utaofanyika Oktoba 31 mwaka huu, sambamba na kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita inayoongoza na Rais Amani Abeid Karume katika nyanja za barabara, huduma za maji safi na salama na elimu.

Wakati huo, leo Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar kwa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein atakwenda kuchukua fomu ya uteuzi wa urais katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), saa 3.00 asubuhi.

No comments:

Post a Comment