Thursday 19 August 2010

WAJANJA WADAIWA KULIPIGI BEI ENEO LA HIFADHI YA BIHOLE.

Wajanja wadaiwa kulipiga bei eneo la hifadhi ya Bihole


Wengine watajwa kuwa wajukuu wa Bihole,


Mjukuu adaiwa kuuza kiwanja 5m/-


Serikali yaombwa kuingilia kati mgogoro



Salum Jecha Na Mandiwa Mgunya, ZJMMC.

SERIKKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeombwa kuingilia kati mgogoro unaofukuta katika eneo la hifadhi, Bungi kwa Bihole, wilaya ya kati Unguja ili kuepusha kuzuka mapambano kati ya pande zinazohusika.

Ombi la kuitaka serikali kuingilia mgogoro huo unaohusu kuuzwa kwa eneo kwenye hifadhi hiyo limetolewa na ushirika wa 'Tusikimbiane' wa kijiji cha Bungi, ukidai eneo hilo la hifadhi limeuzwa bila ushirika huo kupewa taarifa.

Wakizungumza na waadishi wa habari hizi, wanachama hao walimtupia lawama Sheha wa shehia hiyo, Haji Suleiman Issa na Katibu wake, Hassan Haji Suleiman, ambae ni mtoto wake kuwa ndio wahusika wakuu wa kuliuza eneo hilo, na kufanywa kiwanja alichouziwa mtu ambaye hadi sasa hajajulikana na wanaushirika hao na hata mwananchi mwengine yoyote wa kijiji cha Bungi.

Katika hali ya utatanishi zaidi, mzee mmoja maarufu wa kijiji hicho, Miraji Mussa aliyezaliwa mwaka 1939 hapo Bungi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika mwaka asioufahamu yeye akiwa ni Katibu wa ASP (Afro Shirazi Paty) pamoja na Baba yake, ndio waliokuwa wahusika wa ugawaji wa ardhi huko Bungi na anakumbuka eneo hilo lenye mgogoro walikabidhiwa watu wawili, Mzee Ali Makame na Mzee Ramadhan, ambao nao baadae walinyang'anywa.

Katika uchunguzi uliofanyikika, waandishi wetu walimuona, Amour Mohammed Abdalla, mfanyakazi wa Idara ya Maliasili Misitu, katika eneo la Jozani ambae alisema mwaka 1980 alipewa eneo hilo kwa ajili ya kilimo na Mzee, Khamis Kibwesha.

Hata hivyo, Amour alisema ilipofika mwaka 1990, Serikali iliwataka wananchi wote wanaolima ndani ya mita 100 kutoka kwenye Gofu la kwa Bihole kwa pande zote nne, Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini waondoke kwa maelezo kuwa sehemu hiyo ni hifadhi ya Gofu,

Katika hali isiokuwa ya kawaida, Amour alidai kuitwa na Katibu wa Sheha na kukabidhiwa shilingi 120,000 na alipohoji sababu za kupewa fedha na Katibu wa Sheha, hakupata jibu zaidi ya kuambiwa atajuilishwa baadae. Alisema hakuna kilichoendelea zaidi ya watu wa karibu na sheha walimwambia hata wao walimjibu hawajui chochote kuhusu kuuzwa kwa kiwanja hicho.

Wakati huo huo, Sheha wa shehia hiyo, Haji Suleimana Issa akizungumza na waandishi kuhusiana na mgogoro huo, alisema eneo hilo lenye mgogoro linamilikiwa na Mzee Haji Mwinyi wa Bungi, ambaye ni mgonjwa kwa sasa na ni mjukuu wa Bihole.

Aidha, Sheha alisema mmiliki wa eneo hilo amabae ni Mzee Haji Mwinyi alimuuzia kiwanja hicho Rashid Suleiman Kassim kwa Shilingi Milioni tano mbele ya mashahidi Ali Juma Khamisi na Jumanne Shija ambapo waandishi wa habari walifika ofisini kwa Sheha na kuiona hati hiyo ya mauziano ambayo ni karatasi ya kawaida iloandikwa kwa mkono.

Hata hivyo, wajukuu wa Mzee Hji Mwinyi anaedaiwa na Sheha kuwa mmiliki halali wa eneo hilo, ambao ni Amina Mwinyi Mussa na Muhammed Haji Bukheti, walisema Babu yao hakua mjukuu wa Bihole kama alivyodai Sheha isipokuwa Mama yake Mzee Haji Mwinyi alikuwa muhudumu wa nyumba ya Bihole.

Aidha, wajukuu hao walisema, Babu yao hakuwahi kumilikishwa kiwanja katika eneo hilo na wanashangazwa na Babu yao kuhusishwa na uuzwaji wa eneo hilo bila ya yeye kujitambua ambapo walidai babu yao alipewa kiasi cha shilingi laki 500,000 kutoka kwa Sheha ambapo alielezwa kuna kiwanja katika eneo la Bihole kinauzwa bila ya yeye kujua ni kiwanja gani kinachouzwa.

Wajukuu hao walieleza kwamba siku moja walikwenda watu walioambatana na sheha kumpiga Picha Babu yao bila wao kujua madhumuni ya picha hizo ambapo waandishi waliona moja ya picha hizo lakini hawakuelewa kwanini alipigwa picha hiyo ingawa wanafikiria alipigwa kuonesha kuwa yeye ni mjukuu wa Bihole, jambo walilosema limechangia kuuzwa kiwanja hicho.

Ushirika huo wa Tusikimbiane unawanachama 20 pamoja na vijana 10 waliopewa mafunzo ya kutembeza wageni katika eneo hilo, ulioanzishwa 2006 na unadhaminiwa na mradi wa TASAF na MACEMP ambapo kwa sasa umetumia zaidi ya shilingi milioni kumi (10,000,000) kulikarabati jengo hilo kwa kutia dari, milango na madirisha pamoja na choo kwa ajili ya huduma ya hapo.

No comments:

Post a Comment