Wakulima karafuu waiomba ZSTC kuwapatia majamvi
Na Madina Mohamed, ZJMMC, Pemba
WAKULIMA wa zao la karafuu kisiwani Pemba, wameliomba Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), kuangalia uwezekano wa kurejesha mikopo ya majanvi ya kuanikia karafuu, ili kuepusha kuharibika kwa zao hilo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafauti, wakulima hao walisema wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa halisi vya kuanikia karafuu, hali inayowalazimisha kuzianika maeneo yasiyo salama hali inayoshusha kiwango na kusababisha hasara.
Walisema uvunaji wa zao hilo unaendelea vizuri na tayari wanazo za kutosha lakini tatizo hilo ndio kikwazo kwao.
Mkulima Suleiman Abdallah Khalfan mkaazi wa Chumbageni Mkoani, alieleza kuwa zamani katika msimu wa karafuu ZSTC ilikuwa ikiingiza vifaa kama majamvi, magunia na taa kwa kuwauzia au kuwakopesha wamiliki wa mashamba ya karafuu ili kuliokoa zao hilo.
Alifahamisha kuwa tangu kuachwa kwa utaratibu huo, baadhi ya wakulima wanapata usumbufu hasa wakati wa kuanika karafuu zao.
Naye Mohammed Shadhil mkaazi wa Chumbageni Wilaya ya Mkoani, alisema kutokana na kukosa vifaa hivyo, hulazimika kuanika karafuu zao juu ya mapaa ya nyumba zilizoezekwa mabati, mabusati au pembezoni mwa barabara.
"Zamani ZSTC ilikuwa ikitupatia majamvi na magunia ya kuhifadhia japo kwa mkopo lakini sasa hakuna, hivyo tunapata shida sana kuanika", alisema Shadhil.
Asha Kombo Khamis aliyeko katika kambi ya uchumaji wa karafuu kijijini Tumbi alisema, siku hizi wanatumia mikeka na mabusati ambayo hata hivyo hayatoshi kutokana na mrundikano mkubwa wa karafuu ambazo hazina pahala pa kuanikiwa.
"Ukitaka majamvi ununue kwa mtu binafsi na bei ni ghali kwani jamvi moja huuzwa kati ya shilingi 5,000 na 6,000 na hakuna mengi", alifafanua Asha.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba Wizara ya Utalii, Biashara na Uwekezaji kupitia shirika lake ZSTC, kurudisha tena uagiziaji wa vifaa hivyo ili kulinusuru zao hilo ambalo ni muhimu kwao na kwa uchumi wa taifa.
Juhudi za kumapata Naibu Meneja Mkuu wa ZSTC Pemba ili azungumzie suala hilo, hazikufanikiwa na zinaendelea, ingawa taarifa za karibuni zilieleza kuwa, ZSTC iliondoa utaratibu huo kuepuka hasara kama ilivyotokea miaka ya nyuma ambapo wamiliki walikopeshwa na kushindwa kulipa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment