Thursday 19 August 2010

MAELFU WAOMBA UANGALIZI UCHAGUZI MKUU ZANZIBAR.

Maelfu waomba uangalizi uchaguzi mkuu Zanzibar


Na Mwantanga Ame (ZJMMC)

WAANGALIZI zaidi ya 2000 wameomba kushiriki kuangalia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika rasmi Oktoba 31 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Tume ya uchaguzi, Salum Kassim Ali, aliiambia Zanzibar Leo kuwa kumejitokeza idadi kubwa ya maombi ya waangalizi wanaokusudia kuja kuangalia uchaguzi Mkuu ujao.

Alisema sehemu ya maombi hayo ni ya waangalizi wa ndani zikiwemo jumuia za kidini na taasisi binafsi.

Mkurugenzi huyo alisema maombi ambayo yalikuwa yamepokelewa hadi hivi karibuni kutoka taasisi za nje yalifikia zaidi ya 135 huku taasisi za ndani yamefikia zaidi ya 2000.

Alisema kati ya maombi hayo, zimo Jumuia na Mashirika ya Kimataifa ambayo yaliomba kufanyakazi hiyo, tokea upigaji kura ya maoni.

"Hivi sasa faili langu limejaa maombi kwani ni mengi na bado tunaendelea kuyapokea kutoka sehemu mbali mbali," alisema Mkurugenzi huyo.

Alifahamisha kuwa idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na ile ya chaguzi zilizowahi kufanyika hapa Zanzibar.

Mashirika ya kimataifa ambayo yameomba kufanyakazi hiyo ni pamoja na Umoja wa Ulaya, UNDP ambao walifadhili zoezi la kura ya maoni.

Wakati kukiwa na maombi hayo, Mkurugenzi huyo alisema zoezi la uchukuaji fomu kwa wagombea wanaotaka kuwania nafasi za Urais linaenda vizuri kwa wagombea wanaotaka kufanya hivyo.

Alisema Ratiba ya Tume hiyo inatarajia wagombea nafasi hiyo watamaliza zoezi hilo Agosti 30, mwaka huu saa 10 jioni na uteuzi utafanywa Saptemba 2 mwaka huu huku muda wa pingamizi utaanzia Septemba 3 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment