Wednesday 18 August 2010

DK. SHEIN ACHUKUWA FOMU KUGOMBEA URAIS ZANZIBAR,

Dk.Shein achukua fomu kugombea Urais Z'bar



Asema atajitahidi kujenga Z'bar mpya


Ataanza kwa kuboresha uchumi 


Asisitiza kujenga Z'bar yenye umoja bila ubaguzi

Na Mwanajuma Abdi

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohammed Shein jana alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na kuahidi kujenga Zanzibar mpya ya kiuchumi na wananchi kuishi kwa amani bila ya hofu yeyote.

Dk. Shein ambae ni Makamo wa Rais wa Tanzania, alichukua fomu hiyo Makao Mkuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), saa tano asubuhi na baadae kwenda Afisi ya CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, Amani, anbapo alizungumza wanachama wa CCM na wanaomdhamini katika fomu hiyo.

Alitaja baadhi ya mambo muhimu atakayoyashughulikia mara baada ya kupata ridhaa ya wananchi ni kuendeleza kuimarisha uchumi wa Zanzibar ili uweze kukua kwa kasi kubwa na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Aidha, aliwatoa hofu wananchi na wasiwasi katika masuala ya wizi, ujangiri, kurushiwa mawe katika mabati na kurushwa mabomu ya chupa na kusababisha miripuko katika maeneo mengi na kusema hali hiyo ya vitisho haitafanyika .

Alisema atabeba jukumu la kuhakikisha kwamba amani inadumishwa hasa wakati wa kampeni.

Alisema utulivu na amani utaendelea kuwepo na wananchi wa Zanzibar wataishi bila ya kubughudhiwa na kufuata misingi ya haki za binadamu na utawala wa bora.

Alisema Wazanzibari wote ni ndugu na wamoja hivyo hakuna sababu ya watu kuishi kwa kuchukiana, ambapo mkazo zaidi utawekwa katika kukuza umoja, mshikamano, amani na utulivu.

Alisisitiza kwamba, Zanzibar itaendelea kutawaliwa na wazanzibari wenyewe hata siku moja hakutataliwa na mgeni.

Alisema akipewa ridhaa ya kuongoza atashirikiana na vyama vyengine vitavyopata nafasi katika uchaguzi mkuu katika uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuendeleza na kudumisha mshikamano kwa watu wote wa Unguja na Pemba.

Alisema kampeni za uchaguzi za Chama cha Mapinduzi (CCM), zitanadi Ilani na sera zake za nyuma na za sasa zitakazozinduliwa hivi karibuni mjini Dar es Salaam na baadae Zanzibar.

"CCM itaendesha kampeni za kistaarabu hazina matusi wala hakitovisema vyama vyengine na badala yake itashindana kwa hoja katika kuinadi, kuiuza ilani na sera kwa wananchi ili waweze kukipa ridhaa ya kushinda chama chao katika uchaguzi mkuu", alisisitiza Dk. Shein.

Aliwaahidi wana CCM kuwa yupo imara kukitumikia chama hicho na wala hatayumbayumba katika kuzinadi sera na ilani wakati wa kipindi cha kampeni.

Mgombea huyo, alisema atahakiskisha kero za Muungano zitamalizika ili wananchi wa pande zote mbili waweze kufaidika vizuri na matunda hayo, pamoja na kuyaenzi na kuyasimamia matunda ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Mapema Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinyichande alimkabidhi Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Ali Mohammed Shein fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi hiyo katika Afisi za Tume hiyo Maisara mjini hapa.

Alimueleza siku ya mwisho kurejesha fomu hiyo ni saa 10:00 za jioni Agosti 30, ambapo pia mgombea anatakiwa aweke dhamana ya shilingi 2,000,000 siku anayorejesha fomu.

Nae Dk. Shein aliishukuru Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa kuendesha mchakato wa utoaji fomu kwa utaratibu mzuri, ambapo aliahidi kufuata taratibu hizo.

No comments:

Post a Comment