Jamii yakithiri kivunja haki za binaadamu - Mwanasheria
Chanzo kutokuwa na elimu, jinsi ya kuzidai
Na Mwantanga Ame
Jumamosi 11 Disemba 2010
VITENDO vya uvunjaji wa Haki za Binaadam vimeshamiri zaidi ndani ya jamii ikilinganishwa na serikali inavyovunja haki hizo.
Mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, Ali Uki alieleza hayo alipokuwa akitoa mchango kwenye kongamano la kuadhimisha siku ya kimataifa ya Haki za Binaadam lililofanyika katika ukumbi wa EACROTANAL Mjini Zanzibar.
Alisema uchunguzi uliofanywa na kituo cha Huduma za Sheria, umebaini vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu kufanywa zaidi na wanajamii kuliko serikali.
Kongamano hilo lilitayarishwa na Kituo Cha Huduma za Sheria kwa ajili ya kuadhimisha miaka 62 ya siku ya haki za binadamu ambapo liliwashirikisha wadau mbali mbali wakiwemo vyama vya siasa, Wanasheria, Asasi za kiraia,Taasisi Binafsi, na vyombo vya habari.
Mwanasheria huyo alisema, ushahidi unaonyesha kuwepo vitendo vingi vya uvunjifu wa Haki za Binaadam kwenye nyumba nyingi wanazoishi wananchi, hali inayotokana na wanajamii wengi kutojua njia za kupata haki pale zinapokiukwa haki hizo.
"Sehemu kubwa ya haki za binadamu zimekuwa zikivunjwa na watu binafsi na sio serikali inawezekana hili likawa linachangiwa watu hawajui namna ya kudai haki zao",alisema Uki.
Alifahamisha kuwa suala la ubaguzi kwenye nchi nyingi za Kiafrika ikiwemo Tanzania, linaendelea kwenye nyanja mbali mbali ikiwemo ajira ambapo mtu huangaliwa sehemu anayotoka, dini huku waliosoma kuachwa mitaani na kuajiriwa ambao hawana elimu.
Alisema uwepo wa baadhi ya vitengo kwa ajili ya kupima vigezo muhimu vya kuajiriwa kazini kama GSO, ni moja ya vitengo ambavyo vinaweza kutumika kufanya ajira za kibaguzi kwani huweza kupima mwananchi huyu ni wa dini gani ama mzaliwa wa wapi.
Aidha Mawanasheria huyo alilalamikikia baadhi ya vipengele vya Mabadiliko 10 ya Katiba ya Zanzibar, juu ya kipengele kinachozungumzia masuala ya haki za binadamu kesi zake kukomea katika Mahakama za Zanzibar na kutotoa haki kufikishwa katika Mahakama ya Rufaa kama pindipo ikijitokeza kufanya hivyo.
Mapema Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, akifungua kongamano hilo alisema ipo haja ya kufanyika kwa tathimini ambayo itabainisha kama Katiba ya Zanzibar na sheria zake zinakubaliana na misingi ya utoaji wa haki za binadamu.
Waziri Bakary, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepania kuheshimu haki za binadamu, lakini jitihada hizo zinaonekana bado hazijafika pale panapotakiwa na ni vyema kwa Wazanzibari kujitahidi kufanikiwa kwenye utekelezaji wa haki hizo.
Waziri huyo alibainisha jitihada kadhaa zilizochukuliwa na serikali katika kuhakikisha inaboresha misingi ya haki za binaadam, ikiwemo kuheshimu mikataba ya kimataifa 'Beijing Platform for Action', kuweka sheria ya kuwalinda wari na wajane,kuongeza idadi ya wanawake katika Baraza la Wawakilishi kufikia asilimia 40 na kuweka sheria za kumlinda mtoto.
Alisema jambo la msingi ambalo linahitajika kuangaliwa ni kuona vipi mwananchi anajengwa namna ya kutambua haki binaadamu kuwa ni haki zao za msingi na sio kufanywa kama ni fadhila.
Nae Mtoa mada katika kongamano hilo, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu, Joaquine De Mello, alisema kuna changamoto kubwa Tanzania kupambana na tatizo la ubaguzi kwani bado yapo mengi yanayotendeka ndani ya familia tofauti ya za rangi, ngozi urefu na ufupi, jinsia, ujana, uzee, mtoto wa kike na wakiume na wanaume kukabiliana na wanawake.
Kamishna huyo akiyataja changamoto nyengine alisema ni ya utajiri na raslimali, tajiri na maskini, viwango vya elimu, Mamlaka na uwezo, hali za afya na fedheha za kukosa afya kwa wagonjwa wa UKIMWI, ukoma na ugumba au utasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment