Monday, 6 December 2010

UN YAOMBWA KUENDELEA KUISAIDIA ZANZIBAR,

UN Yaombwa kuendelea kuisaidia Zanzibar



Na Abdi Shamnah


Jumatatu 6 Disemba 2010

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ameuomba Umoija wa Mataifa kuendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar ili iweze kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Maalim Seif alitoa ombi hilo jana ofisini kwake Migombani wakati alipozungumza na Mwakilishi mkaazi wa Umoja wa Mataifa aliopo Zanzibar,Kana Sorro.

Amesema Umoja wa Mataifa kupitia Shirika la Global Funds limekuwa likitoa misaada mbali mbali kwa Zanzibar, ikiwemo ya kifedha kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi pamoja na Malaria.

Hata hivyo, alisema 2007 katika awamu ya kwanza ya misaada hiyo ya kipindi cha miaka miwili, Shirika hilo lilisititisha misaada yake kwa Zanzibar, na badala yake kutoa Dola 135,000 ikiwa ni msaada wa mwaka mmoja pekee (2007/08).

Kufuatia hali hiyo Maalim Seif alimuomba Mwakilishi huyo kuangalia uwezekano wa kuwepo misaada endelevu kwa Zanzibar, kwa kuzingatia kuwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti ongezeko la ugonjwa huo kwa wastani wa asilimia 0.6.

Alimweleza Mwakilishi huyo kuwa uwepo wa makundi hatarishi yanayoishirikisha zaidi nguvu kazi ya Taifa, kunatishia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Alisema Serikali kupitia ofisi yake imejizatiti kiikamilifu kukabiliana na maambukizi na ugonjwa wa ukimwi sambamba na matumizi ya madawa ya kulevya.

Aidha Maalim Seif alimuomba Mwakilishi huyo kuangalia uwezekano wa kusaidia Zanzibar katika njia za kukabiliana na athari za kiimazingira zinazozikabili fukwe hapa nchini.

Alisema hali ya kimazingira katika fukwe, hususan zile ziliopo katika ukanda wa Kusini Mashariki ya Bahari ya Hindi ni mbaya, ambapo maji ya chumvi yamekuwa yakimega ardhi ya kisiwa hiki kila kukicha.

Katika hatua nyuingine Maalim Seif aliiomba UN kuangalia njia za kuweza kuisaidia Zanzibar kuimarisha Daftari lake kiutawala, akianisha kuwepo kwa kasoro kubwa katika daftari hilo, ambapo baadhi ya Wazanzibari wenye sifa wamekosa kuandikishwa, hali iliopelekea kukosa kupiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita.

Nae Mwakilishi wa UN nchini, Kana Sorro, alimhakikishia Makamu wa kwanza wa Rais kuwa mapendekezo hayo ameyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi.

No comments:

Post a Comment