Friday, 10 December 2010

KETE MBILI ZA DAWA ZA KULEVYA ZAMFIKISHA MAHAKAMANI.

Kete mbili za dawa za kulevya zamfikisha mahakamani



Na Said Abdu-rahman, Pemba
Alhamisi 9 Disemba 2010

MAHAKAMA ya Wilaya Wete imempeleka rumande wiki mbili kijana mmoja mkaazi wa Chasasa anayekabiliwa na mashitaka ya kupatikana na dawa za kulevya kinyume na sheria.

Mshitakiwa huyo Juma Khamis Juma (19), ambae alifikishwa Mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa shitaka lake hilo.

Akiwa Mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nyange Makame, Mwendesha Mashitaka kutoka Jeshi la Polisi Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, Massoud alimsomea mshitakiwa hiyo kosa linalomkabili.

Alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 16(1)(a) sheria No, 9 ya mwaka 2009, sheria ya Uingizaji na Matumizi ya Dawa haramu, sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa hati ya maelezo ya mashitaka iliyowasilishwa Mahakamani hapo na kusomwa na Mwendesha Mashitaka huyo, ilidai kuwa shitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya aina ya heroine kete mbili ndani ya kibiriti zenye uzito wa gramu.

Alifahamisha kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 6 mwaka huu majira ya saa 5:00 za asubuhi huko Bopwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu lolote Mahakamani hapo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Baada ya Maelezo hayo Mwendesha mashitaka Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, alimuomba Hakimu Nyange kuliahirisha shauri hilo na kulipangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusomwa Mahakama inayohusika.

Hakimu Nyange alikubaliana na ombi la Mwendesha Mashitaka na hivyo kuiahirisha kesi hiyo hadi Disemba 20 mwaka huu ambapo kesi hiyo itasikilizwa katika Mahakama ya Mkoa .

No comments:

Post a Comment