Zanzibar imepiga hatua kubwa kuwapa elimu watoto – Waziri Shaaban
Na Mwanajuma Abdi
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikiipa kipau mbele sekta ya elimu pamoja na kukuza kiwango cha elimu kwa skuli za maandalizi na msingi, ili watoto wawe na makuzi mazuri ya hapo baadae.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ramadhan Abdallah Shaaban, alisema jana alipokuwa akifungua mkutano wa siku tatu wa kimataifa wa malezi na maendeleo ya watoto, uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini nje kidogo wa mji wa Zanzibar.
Mkutano huo wa kwanza wa aina yake kufanyika Zanzibar ambapo mwaka jana ulifanyika Dakar, Senegal, unawahusisha washirikia kutoka katika Mashirika ya Kimataifa yanayohusiana na maendeleo ya watoto.
Waziri Shaaban alisema serikali ya Mapinduzi imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha watoto wanapata elimu, huku ikiwa tayari imefikia hatua ya malengo ya milenia.
Aidha alisema Zanzibar imepitisha sera ya elimu mwaka 2006, ambayo itoa kipaumbele kwa elimu ya lazima ya miaka miwili ya maandalizi ya mtoto kabla ya kuingia msingi katika kuwajengea uwezo na upeo mkubwa wa ufahamu wa elimu.
Alifahamisha kuwa, Serikali imejidhatiti katika kukuza maendeleo ya watoto katika familia, kwa kupambana na umasikini na kukuza uchumi (MKUZA) na dira ya 2020 ili waweze kulinda na kupatiwa mahitaji muhimu ikiwemo lishe bora ili aweze kukuwa vizuri.
Waziri Shaaban alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kusaini mkataba wa kimataifa wa kulinda haki ya mtoto katika kulinda na kuwajengea makuzi mazuri katika elimu, afya na mambo yote muhimu yanayowahusu wao.
Hata hivyo, alieleza Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kupungua vifo vya akinamama wajawazito na watoto waliokuwa chini ya umri wa miaka mitano pamoja na kupambana na malaria.
Katibu Mkuu wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mwanaidi Saleh Abdulla alisema amefarajika kuona mkutano huo umefanyika Zanzibar na utasaidia kutoa muamko wa jamii katika kulea watoto vizuri sambamba na vituo vya maandalizi ambapo ndio msingi wa elimu unapoanzia.
Nae Rokhaya Diawara anayefanya kazi na makundi ya Mashirika mbali mbali ya kimataifa la ADEA, ECD, UNESCO BREDA, aliwahimiza washiriki hao wafanye kazi kwa pamoja katika malezi na maendeleo ya mtoto katika Bara la Afrika na duniani kote.
Alisema kuwepo kwa mawasiliano ya mara kwa mara ndio njia pekee ya kuwasaidia maendeleo ya watoto tokea wanapokuwa tumboni hadi wanapofikia umri wa miaka minane, ambapo ndio muda muafaka katika kuwatunza na kuwapa lishe bora na afya ili wawe na makunzi mazuri ya kiakili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment