Friday 10 December 2010

WAZIRI WA MIUNDOMBINU AZUIA SAFARI ZA MELI YA MV MAENDELEO.

Waziri wa Miundombinu aizuia safari za MV Maendeleo

Na Raya Ahmada, Pemba
Jumamosi 11  Disemba 2010

WAZIRI wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Massoud ameizuia meli ya M.V Maendeleo kuendelea na safari zake za kawaida za kubeba mizigo na abiria.

Waziri huyo amelazimika kuzuia safari za meli hiyo, kutokana na kuharibika mashine yake moja ikiwa kwenye safari zake hali iliyosababisha kufungwa tagi na kukokotwa hadi bandarini Mkoani.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masuod Hamad alitoa agizo hilo mbele ya manahodha na mafundi wa meli hiyo huko bandarini Mkoani, akiwa katika ziara zake za kuyatembelea Mashirika na Idara zilizomo katika wizara hiyo kisiwani Pemba.

Waziri huyo alisema hatua ya kuzuiliwa safari za meli hiyo inatokana na kuharibika mara mbili wakati ilikiwa kwenye safari zake za Unguja na kuifanya meli hiyo itembee ikiwa na mashine moja.

Alisema serikali inajali na kuthamini maisha ya wananchi wake na wala haitakubali kuona meli hiyo inasafirisha abiria ikiwa inatembea na injini moja kama ilivyokuwa ikifanya.

“Meli ipelekwe Mombasa ikatengenezwe injini zote mbili ndio ifanye kazi za kupakia abiria”, alieleza.

Akizungumza na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa wakati tofauti, aliwataka wakuu wa vitengo kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na sio kujenga woga kwa kuwaogopa wakubwa wao au kufata matakwa yao.

Nae Naibu waziri wa wizara hiyo Issa Haji Usi, alisema lengo walilojipangia ni kufanya mabadiliko kwa kuifanya wizara hiyo kuwa ya mfano katika utoaji wa huduma za uhakika kwa jamii.

Nae fundi mkuu wa meli ya M.V. Maendeleo alikiri kuharibia meli yao wakati wameshaingia katika maeneo ya kisiwa cha Pemba na kusaidiwa na tagi ya mpaka kwenye gati ya Mkoani.

Hiyo ni ziara ya kwanza kwa waziri wa Miundombinu na Mawasiliano na Naibu wake kutembelea Mashirika na Idara za wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment