Friday 10 December 2010

DEREVA ALIPA FAINI KUKWEPA CHUO CHA MAFUNZO

Dereva alipa faini kukwepa Chuo cha Mafunzo



Na Khamis Amani
Alhamisi 9 Disemba 2010


DEREVA wa gari ya abiria yenye nambari za usajili Z 745 AY, amenusurika kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita, baada ya kulipa faini ya shilingi 70,000.

Faini hiyo ameilipa baada ya kutiwa hatiani na mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe, dhidi ya kesi ya kuendesha gari ya abiria ikiwa leseni ya udereva haimruhusu.

Abdallah Kweli Juma (26) mkaazi wa Amani wilaya ya Mjini Unguja, amepatikana na hatia hiyo, baada ya kukubali kosa hilo mbele ya hakimu Janet Nora Sekihola alikofikishwa kujibu shitaka hilo.

Mara baada ya kukubali kosa hilo lililowasilishwa na Mwanasheria wa serikali Khamis Jaffar Mfaume, kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), mahakama hiyo ilimtaka kulipa faini ya shilingi 70,000 au kutumikia Chuo hicho cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, huku mshitakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo imsamehe, upande wa mashitaka kwa upande wake uliomba itolewe adhabu kwa mujibu wa maelekezo na kudai kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya zamani juu yake.

Awali akiwa mahakamani hapo ilidaiwa kuwa, kinyume na kifungu cha 102 (a) (b) cha sheria namba 7/2003 sheria za Zanzibar, mshitakiwa huyo alipatikana akiendesha gari ya abiria iendayo njia namba 505 ikiwa leseni yake ya udereva haimruhusu.

Mahakama ilifahamishwa kuwa, kisheria alitakiwa kuwa na leseni ya class D, badala ya class DI aliyokuwa akiitumia shitaka ambalo alilikubali mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment