Friday 10 December 2010

DEREVA KIZIMBANI KWA KUTOFUNGA MKANDA

Dereva kizimbani kwa kutofunga ukanda




Na Khamis Amani
Alhamisi 9 Disemba 2010

MKAAZI mmoja wa Amani wilaya ya Mjini Unguja, ambaye ni dereva wa gari ya abiria iyendayo njia namba 501 yenye nambari za usajili Z 584 CG, amefikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe kwa kosa la kushindwa kufunga ukanda wa usalama.

Mshitakiwa huyo Yussuf Mohammed Juma (27), amekubali kosa hilo mahakamani hapo, na kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.

Adhabu hiyo dhidi yake imetolewa na hakimu Janet Nora Sekihola, mara baada ya kukubali kosa hilo alilosomewa na Mwendesha Mashitaka Khamis Jaffar Mfaume, Mwanasheria wa serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakati Mwanasheria huyo wa serikali kuomba itolewe adhabu kwa mujibu wa sheria kwa madai hawana kumbukumbu za makosa ya zamani dhidi yake, kwa upande wake mshitakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo imsamehe.

Hakimu Janet Sekihola baada ya kupitia hoja za pande mbili hizo, alimtaka mshitakiwa huyo kulipa faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo hicho kwa muda wa miezi mitatu, faini ambayo aliilipa mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo alidaiwa kushindwa kufunga ukanda wa usalama, wakati akiendesha gari hiyo alipokuwa akitokea upande wa Kwabiziredi kuelekea upande wa Michenzani.

Kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 130 (2) (4) cha sheria namba 7/2003 sheria za Zanzibar, lilidaiwa kutokea Kariakoo wilaya ya Mjini Unguja, saa 2:45 za asubuhi ya Disemba 5 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment