Tuesday, 7 December 2010

MTAMBO WA KISASA WAKUWASHIA TAA UWANJA WA NDEGE WAFUNGWA.

Mtambo wa kisasa wakuwashia taa uwanja wa ndege wafungwa


Na Mwanajuma Abdi
Jumanne 7 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imefunga mtambo wa kisasa uitwao SCADA wa kuwashia taa unaotumia mtandao wa komputa katika barabara ya kurukia na kutulia ndege ya kiwanja cha Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa Idara ya Anga, Malik Mohamed Hanif, alisema mtambo wa SCADA ni wa kwanza kufungwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Alisema mtambo wa SCADA unatumiwa katika kuwasha taa katika barabara ya kurukia ndege na kutulia kwa nyakati za usiku na mchama ili kusaidia kuongoza vizuri ndege wakati inapofika katika Uwanja huo ikiwa angani.

Alieleza mtambo huo unaendeshwa kwa mtandao wa komputa unasaidia kurahisisha kazi iwapo taa zikiwa haziwaki katika eneo lolote linalozunguka katika barabara hiyo.

Aidha alisema awali uwanja huo ulikuwa unatumia mtambo wa MIMIC ambao ulikuwa unatumia 'swich' za kuwacha kwa kawaida, ambapo hata kama taa zitakuwa zinamatatizo sio rahisi kuonyesha kama hazikwenda kuangaliwa.

Alifahamisha kuwa, lakini tokea kufungwa kwa mtambo wa SCADA kila kitu kinajionesha katika kompyuta iwapo kutatokea hitalafu au kutowaka kwa taa katika kiwanja hicho.

Mkurugenzi huyo, alisema Uwanja huo unaendelea kuimarishwa baada ya kukamilika matengenezo upanuzi wa njia ya kurukia na kutulia ndege, ili kwenda sambamba na hadhi ya kimataifa na kuweza kuyavutia mashirika mbali mbali ya kimataifa.

Alifahamisha kuwa, hivi sasa ujenzi wa ukuta wenye urefu wa kilomita 12 unandelea, ambao utatumia jumla ya shilingi bilioni tano hadi kukamilika kwake.

Kuimarishwa kwa Uwanja huo utasaidia kuongeza mapato ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia safari za anga kwa kuongeza idadi ya ndege na watalii wengi kuja kutembelea nchini na wenyeji nao kutumia huduma hizo zilizokuwa bora kwa ajili ya kusafiri na kufanya biashara.

No comments:

Post a Comment