Sunday, 5 December 2010

RAIS KIKWETE : BIASHARA, UWEKEZAJI UMEKUWA AFRIKA MASHARIKI.

Rais Kikwete: Biashara, Uwekezaji umekua Afrika Mashariki


 Ataka miundombinu iimarishwe kuvutia wawekezaji


 Nkurunzinza asisitiza kuimarishwa demokrasia

Na Omar Said, Arusha


Jumapili 5 Disemba 2010

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kiwango cha biashara na uwekezaji kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, kimeongezeka kwa asilimia 40 kutoa mwaka 2005 hadi mwaka jana, hali inayoonyesha kukua kwa uchumi wa nchi hizo.

Dk. Kikwete alisema hali hiyo inatokana na juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha vikwazo na usumbufu kwa wafanyabiashara na wawekezaji vinapatiwa ufumbuzi ili kuharakisha maendeleo.

Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa 12 wa viongozi Jumuiya ya Afrika Mashariki, huko Ngurdoto nje kidogo ya jiji la Arusha, wakati akimkabidhi Uenyekiti wa Jumuiya hiyo Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.

Dk. Kikwete alisema kuongezeka kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwenye mataifa hayo kunahitaji kuendelezwa na kuhakikisha vikwazo na malalamiko yanayohusu sekta hizo yanaondolewa.

Aliongeza kuwa ni lazima mafanikio yaliyoanza kupatikana yanaendelezwa kikamilifu, kwani woga uliokuwepo katika ushuru wa forodha kati ya Uganda na Tanzania haupo tena, hivyo mataifa hayo yanaongeza mapato kwenye biashara, ambapo yalikuwa yanaigopa Kenya sasa wanaaminiana.

Alisema kwa mfano Uganda imefanikiwa kuingiza kutoka Kenya kutoka dola 15.5 milioni mwaka 2004 hadi kufikia 135 mwaka 2009, hali inayoashiria uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki umeanza kutoa matunda mazuri.

Alisema Tanzania imeuza Kenya bidhaa zenye thamani ya kuridhisha, ambapo imeongezeka hadi kufikia dola 300 za Marekani mwaka 2009 kutoka 95.5 dola za Marekani kipindi cha 2004.

"Ni vyema sekretarieti ikahakikisha inachukua hatua za kuondoka vikwazo vyenye kutatiza biashara na uwekezaji kwenye nchi wanachama”,alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete aliridhishwa na makampuni ya nchi hizo kuwekeza ndani ya nchi za ukanda huo akitolea mfano kampuni ya Azam ya Tanzania, ambayo imewekeza viwanda mbalimbali vya usagishaji wa bidhaa katika nchi za Rwanda, Kenya, na Uganda.

"Ni matarajio yangu kwamba kukua kwa uwekezaji ndani ya nchi wanachama kutaweza kuimarisha sekta mbalimbali zikiwemo za fedha, bima na elimu, ambapo kufunguliwa kwa soko la pamoja kutainua na kusaidia kukua kwa shughuli za kibiashara”,alisema Rais Kikwete.

Kwa upande mwengine Rais Kikwete alisema katika kipindi hicho, Jumuia hiyo imekumbana na changamoto kadhaa zikiwemo za kutokuwa na bajeti ya kuridhisha kulikosekana kwa taarifa sahihi za kitakwimu kwenye sekta ya biashara na uwekezaji na kutokupatiakana habari kwa mtiririko wa kuridhisha.

Aidha Rais Kikwete alisema Afrika Mashariki kuna matatizo mengi hasa ukosefu wa miundombinu mizuri inayoweza kuwavutia wawekezaji na kueleza kuwa mikakati inahitajika katika kuhakikisha hali hiyo inapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo Rais Pierre Nkurunziza, alisema ni lazima nchi wanachama ziongeze demokrasia ili wananchi washiriki kikamilifu kwenye sekta mbalimbali zinazowahusu.

"Jumuiya ya Afrika Mashariki lazima iwe muangalizi wa demokrasia katika nchi wanachama ambapo ijiridhishe mafanikio na kukubali kwamba zoezi la kuongeza demokrasia linawanufaisha walengwa”,alisema Rais Nkurunzinza.

No comments:

Post a Comment