Sunday 19 December 2010

UNICEF YAPONGEZA MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UDHALILISHAJI

UNICEF yapongeza mikakati ya kupambana na udhalilishaji

Na Sharifa Maulid
Jumatatu 20 Disemba 2010
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), limesema litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika utekelezaji wa programu zake mbali mbali kwa lengo la kumuhifadhi mtoto.

Mwakilishi mkaazi wa UNICEF Zanzibar, Ruth Leano alieleza hayo alipokuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Rahma Mohammed Mshangama huko afisini kwake Mwanakwerekwe mjini Zanzibar.

Mwakilishi huyo alisema Shirika hilo kupitia programu zake litafanya kila iwezekanavyo kusaidia watoto wa Zanzibar.

Alisema hivi sasa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mtoto hasa kwa kuundwa kwa kamati za kupambana na udhalilishaji wa kijinsia kuanzia ngazi ya chini hadi taifa pamoja na utayarishaji wa sheria ya mtoto Zanzibar.

Ruth alisema watendaji wa kitengo cha uhifadhi wa mtoto kutoka shirika lake wameshauri kuingizwa masuala ya watoto katika programu mbali mbali nchini ikwemo Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Rahma Mshangama alisema kuunganiswa kwa Wizara yake na Idara ya Ustawi wa Jamii iliyokuwa wizara ya Afya ni hatua nzuri ya kuleta ufanisi wa kumlinda na kumuhifadhi mtoto nchini.

Kuhusu rasimu ya sheria ya mtoto Zanzibar alisema mwamko zaidi unahitajika kwa wadau mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini na wajumbe wa baraza la Wawakilishi, hivyo ameliomba shirika la UNICEF kutoa ushirikiano wake ili kuweza kutekeleza hatua iliyofikiwa.

Katibu huyo ameliomba Shirika hilo na wadau wengine kuwawezesha wazazi kiuchumi katika kubuni na kuendesha miradi ili kunyanyua vipato vyao jambo ambalo litasaidia kupunguza ajira za watoto nchini.

“Katika kupambana na udhalilishaji wa kijinsia ujumbe kutoka Zanzibar ulioshirikisha watendaji wa Wizara yangu, Polisi, Mkurugenzi wa mashtaka, Mahakama, watendaji wa ustawi wa jamii pamoja na wadau wengine walikwenda nchini Zambia kuangalia wenzetu wamefanya nini katika kupambana na tatizo hilo, hivyo ripoti ya ziara hiyo itasaidia sana Zanzibar kwenye utekelezaji wa kuondosha tatizo hilo”,alisema.

No comments:

Post a Comment