Wednesday, 1 December 2010

DK.SHEIN :TANZANIA IJIDHATITI KUFAIDIKA NA AZIMIO LA TIPOLI.

Dk.Shein: Tazania ijidhatiti kufaidika na Azimio la Tipoli


 Ana matumaini makubwa ushirikiani Afrika, Ulaya

 Fursa za ndani, nje zitumiwe vyema

Na Mwantanga Ame
Alhamisi,2 Disemba 2010




TANZANIA ina matumaini makubwa ya kuweza kufanikisha malengo ya milenia kupitia Azimio la Mkutano wa Tripoli kwa kutekelezwa Mkakati wa utekelezaji azimio hilo.

Azimio hilo limepishwa kwa pamoja kati ya Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Afrika, kwenye Mkutano wa tatu wa ushirikiano baina yao (EU-AU SUMMIT) uliomalizika juzi Mjini Tripoli, Libya.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kiwanja cha ndege cha Zanzibar alipowasili nchini akitokea Tripoli Libya kushiriki mkutano huo, akimwakilisha Rais wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Alisema kupitia Azimio la Tripoli serikali ya Tanzania na serikali ya Zanzibar imejenga matumaini makubwa ya kuweza kuleta mabadiliko ya kufanya vizuri katika utekelezaji wa malengo ya milenia na mipango yake mingine ya maendeleo na kinachohitajika kuwepo kwa mkakati imara wa utekelezaji wake ndani ya nchi na michango ya kweli kutolewa na washirika wa maendeleo kwa kila sekta.

Alisema mchango wa Watanzania na wafadhili utakuwa muhimu kwa vile maazimio hayo ni yenye uwezeshaji mzuri, kwani yataimarisha masuala ya Usalama katika bara la Afrika, Haki za binadamu, Utawala bora, Uhamiaji, kukuza uchumi, uwekezaji, kubuni njia za ajira na ushirikiano wa kikanda.

Mambo mengine aliyataja ni pamoja na suala la Mitandao ya Nishati, Ulinzi Mipango ya milenia, Mazingira ambapo utekelezaji wake umepangwa kwa miaka mitatu.

Alisema katika mkakati huo masuala ya misaada na taaluma na nyenzo katika kuimarisha kilimo na uwekezaji yamepewa kipaumbele.

Akizungumzia ufinyu wa bajeti za Tanzania, Dk. Shein amesema ni lazima kufanyike utekelezaji makini kama ilivyopangwa kibajeti, huku washirika wa maendeleo nao watoe mchango kusaidia utekelezaji wa mkakati huo.

Alisema ni muhimu kuendelea kupatiwa misaada, kwani hivi sasa bajeti ya Tanzania imekuwa ikipata mikopo kwa asilimia 20 huku misaada ikiwa inafikia aslimia 30, lakini kubwa linalolazimika kufanywa kuona maazimio yaliofikiwa katika kikao hicho yanatekelezwa ni kuandaa mkakati madhubuti na kusimamiwa utekelezaji wake.

Alifahamisha ili mikakati hiyo iweze kupata mafanikio ni juu ya suala ambalo litahusisha usimamizi wa kuwa na nyenzo muhimu ambazo zitaweza kukuza utoaji wa huduma katika sekta zote muhimu hasa zile ambazo zimeandaliwa kwa mahitaji ya jamii.

Akitaja mahitaji hayo alisema ni katika suala la kutumia zaidi kilimo cha umwagiliaj, mbegu bora, kuzalisha, kuwa na watalamu ugani kutoa taaluma kwa wakulima na nyenzo kwa vile tayari mkutano huo umebaini mambo hayo kuwa ni ya msingi kutekelezwa ili kuweza kufanikisha malengo.

Aidha alisema kuna haja ya wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania kuwezeshwa ili waweze kuvuka mipaka zaidi ya masoko ya Afrika Mashariki, SADC na Afrika kwa jumla na badala yake wafike Ulaya na kwengineko jambo ambalo linahitaji ushirikiano mkubwa baina ya Jumuiya ya Afrika na Ulaya, kama ilivyoelezwa katika mmkutano huo wa Tripoli.

Dk. Shein, katika kiwanja cha Ndege cha Zanzibar alipokewa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Abdalla Mwinyi Khamis, na Mawaziri na Makatibu wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wengine waliompokea katika kiwanja hicho cha Ndege ni pamoja na wazee wa Chama pamoja na wanachama wa CCM, na kutumbuizwa na ngoma asilia.

Katika ziara hiyo ambayo Dk. Shein alimuwakilisha Dk. Kikwete, aliongoza ujumbe wa viongozi mbali wa Tanzania, akiwemo Waziri wa Nchi Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Dk. Mohammed Maundi na Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za kimataifa katika wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa.

Naye Rajab Mkasaba anaripoti kutoka Tripoli Libya, Makamu wa Rais wa Kenya, Kalonzo Musyoka amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Pongezi hizo amezitoa alipokuwa na mazungumzo na Dk.Shein mjini Tripoli, Libya ambako viongozi hao wote walihudhuria katika mkutano wa tatu wa Mashirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Ulaya.

Katika mazungumzo hayo Musyoka alitoa pongezi kwa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi kwa amani na utulivu na kuweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa Kenya itaendeleza uhusiano na Zanzibar ambao upo kwa muda mrefu.

Nae Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais Kibaki kutokana na salamu za pongezi alizomtumia kutokana na kuchagiliwa kwake kuwa Rais wa Zanzibar na kumueleza Musyoka kumfikishia kiongozi huyo salamu za shukurani kutoka kwake.

No comments:

Post a Comment