Wednesday, 1 December 2010

KUBADILI TABIA SILAHA YA KUMALIZA UKIMWI.

‘Kubadili tabia silaha ya kumaliza UKIMWI’


Mwanajuma Abdi


Alhamis 2 Disemba,2010
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar inakabiliwa na changamoto za vishawishi vinavyoweza kuongeza kasi ya maambukizi ya UKIMWI.

Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi aliyasema hayo jana, Hoteli ya Bwawani mjini hapa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, ambapo alimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Balozi Iddi alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na utandawazi, kupanuka kwa huduma za mawasiliano ambazo zinaonyesha kila aina ya vitendo vinavyoweza kushawishi watu kuchangia katika kuenea maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Makamu huyo alisema kuimarika kwa sekta ya utalii na uingiaji wa wageni wa aina mbali mbali nchini nalo pia linaweza kuchangia uenezaji wa UKIMWI kama ilivyotokea kwa baadhi ya nchi nyengine, huku pia akilielezea tatizo la kuporomoka kwa maadili ya vijana.

Alisema nchi inahitaji maendeleo hivyo ni vigumu kusitishwa kwa harakati za aina hiyo kwa kuhofia maambukizi ya UKIMWI, ila mkazo uwekwe katika kuielimisha jamii juu ya madhara hayo na kuheshimu mila na maadili ya Zanzibar.

Alieleza njia ya kukabiliana na UKIMWI ni kubadili tabia na hizo zinazotajwa kuwa zinaweza kudhibiti maradhi hayo ni za kubahatisha kwa kutokuwa na uhakika.

"Maambukizi ya UKIMWI yanatokea miongoni mwa watu wa rika zote, wakiwemo hata watoto wa chini ya miaka mitano, taarifa za Kitengo cha Kudhibiti UKIMWI cha Wizara ya Afya zimeonyesha watoto wa chini ya miaka 15 waliosajiliwa katika vituo vinavyotoa huduma na tiba ya maradhi haya ni 428 kati ya hao 225 wanaume na wanawake 203 na wengine wameanza kutumia dawa za ARV watoto 227", alieleza Balozi Iddi.

Makamu huyo alisema ni mwaka wa 24 tokea UKIMWI kugundulikana nchini, ambapo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua mbali mbali kuhakikisha gonjwa hilo halienei pamoja na kuendelea kutoa huduma za tiba.

Aidha alifahamisha kuwa, asasi zisizo za Kiserikali nazo zimefanya kazi nzuri katika mapambano dhidi ya maradhi hayo pamoja na hatua mbali mbali.

Alizitaja hatua hizo ni pamoja na kutolewa kwa misaada ya fedha na isiyo ya kifedha ikiwemo chakula, sare na vifaa vya skuli kwenye familia ambazo zinatunza watoto yatima na wengine wanaoishi katika mazingira magumu.

Makamu huyo alipingana na wale wanaoendeleza unyanyapaa kwa watu wenye virusi vya UKIMWI, na kusema kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, ambapo Zanzibar kupitia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia mikataba ya kuheshimu haki za binadamu.

Mapema Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, alisema asilimia kubwa ya wanajamii wa Zanzibar wanaelewa athari za ugonjwa huo, hivyo aliwasihi waache kuwabagua walioambukizwa.

Aidha alimpongeza Balozi wa hiari wa mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar, Mke wa Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Shadya Karume kwa kuwa mstari wa mbele kupiga vita maradhi hayoa nchini.

Nae Mwakilishi wa UNICEF Dorothy Rozga alisema kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo Zanzibar kimebakia ni kidogo kwa miaka mingi na alishauri jamii iache kuwanyanyapaa na kuwabagua watu wanaoishi na VVU.

Nae Makamu Mwenyekiti wa Tume ya UKIMWI Zanzibar, Nasima Haji Chum, alisema tafiti zinaonyesha kwamba maambukizi ya UKIMWI yanasababishwa na biashara za ngono kwa asilimia 10.8, wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao asilimia 12.3 na wanaotumia dawa za kulevya asilimia 16.

Kilele cha maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani hufanyikia kila ifikapo Disemba Mosi ambapo ujumbe wa mwaka huu 'Zuia UKIMWI timiza ahadi'.

No comments:

Post a Comment