Sunday, 5 December 2010

MAALIM SEIF TIJA YA UTALII LAZIMA IWAFIKIE WANANCHI.

Maalim Seif: Tija ya utalii lazima iwafikie wananchi• Rushwa uwanja wa ndege yaliza wawekezaji


Na Khamis Mohammed


Jumapili 5 Disemba 2010

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na ZATI ili kuhakikisha utalii unaendelea kuleta tija kwa Zanzibar na wananchi kwa ujumla.

Hayo aliyasema wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Jumuiya hiyo ya Wawekezaji Sekta ya Utalii Zanzibar huko hoteli ya The Sea Cliff and SPA Zanzibar, Mangapwani wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Maalim Seif, alisema serikali pia itahakikisha inaweka miundombinu ya kisasa ambayo itawavutia wawekezaji wa sekta ya utalii kuwekeza zaidi visiwani hapa.

Alisema ingawa hivi sasa miundombinu ya barabara, mawasiliano na huduma nyengine tayari zimeenea katika maeneo ya utalii, lakini huduma hizo zitaongezwa zaidi ili kuufanya utalii endelevu.

“Ni kiasi cha dakika 45 tu unachukua hivi sasa ili kufika maeneo mengi ya utalii, ni hatua kubwa tumeshaifikia”, alieleza Makamu wa Rais.

Alisema mbali na kuimarishwa kwa barabara, lakini pia huduma za uwanja wa ndege nazo zimeimarika na hivyo kuongeza chachu kwa watalii kufika Zanzibar.

“Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya kutua na kurukia ndege bila ya shaka kutazifanya ndege kubwa kutua, ni faraja kwa Zanzibar”, alisema.

Aidha alisema kupelekwa kwa umeme Pemba hivi sasa pia kutaongeza idadi ya wawekezaji wa utalii katika kisiwa hicho na kupanua sekta hiyo.

Pia Makamu wa Rais, alielezea haja ya kuendelea kuwepo kwa amani na utulivu ili kuifanya biashara ya utalii izidi kupiga hatua.

Mapema Mwenyekiti wa ZATI, Simai Mohammed Said, alisema jumuiya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi na Serikali.

Alizitaja changamoto hizo ni pamoja na suala zima la usalama wa wageni katika maeneo kadhaa zikiwemo fukwe sambamba na kero za mapapasi.

Alifahamishwa kuwa mapapasi kwa njia moja au nyengine wanachangia kuleta taswira mbaya kwa watalii wanaotembelea visiwa hivi.

Aidha alisema vitendo vya rushwa katika uwanja wa ndege wa Zanzibar navyo vinaiweka sekta ya utalii katika hatari ya kupoteza wageni na hivyo kushusha wingi wa wageni.

Hivyo, Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa Serikali kupanga mikakati madhubuti itakayohakikisha sekta ya utalii inaendelea kuchangia pato la taifa kwa kutoa huduma za uhakika za uwekezaji wa sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment