Tuesday 7 December 2010

SHEKH SORAGA ATAKA WAISLAMU WAWAJIBIKE.

Sheikh Soraga ataka waislamu wawajibike



Na Mwantanga Ame


Jumanne 7 Disemba 2010

WAISLAMU na wametakiwa kusherehekea mwaka mpya wa kiislamu huku wakitambua wanajukumu la kutoa mchango wa kuwajibika katika serikali mpya ya Zanzibar, ili kuifanya kuwa ni yenye neema katika mwaka ujao.

Katibu wa Afisi wa Mufti ya Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga aliyasema hayo jana katika salamu zake kwa waumini wa dini ya kiislamu na Wazanzibari wote katika kuadhimisha mwaka mpya wa Kiislamu.

Mwaka mpya wa kiislamu kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu unatarajiwa kuanza leo ambapo ni mwaka 1432 (HIJRIA).

Katibu huyo alisema kutokana na Zanzibar kuwa ipo katika hali ya amani na utulivu baada ya kumalizika kwa zoezi la uchaguzi Mkuu, ni vyema waumini wa dini ya kislamu na wakaelewa kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushiriki kufanya kazi kwa bidii.

Katibu huyo alisema kuwa kila Mzanzibari aliyepata nafasi ya kuwaongoza wenzewe ahakikishe kuwa anatumiwa nafasi aliyopewa kwa uadilifu na kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia wananchi.

Alisema suala la kuipembejea kazi yake, kuwa muaminifu na kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi ni moja ya mambo ya msingi yanayohimizwa katika dini na ni haramu kwa mtu kupokea mshahara ambao hakuufanyia kazi.

Sheikh Soraga alisema jambo la msingi ambalo waislamu wanatakiwa kuzingatia ni kuhakikisha mwaka mpya ulioingia unawajengea mapenzi na mshikamano na viongozi waliopo madarakani bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.

Aidha katibu huyo aliiomba jamii kuimarisha maadili kwa vijana wa Zanzibar kwa maslahi ya nchi na vizazi vijavyo kwani ndio wanaotegemewa kulijenga taifa hili hapo baadae.

Alisema Zanzibar yenye mabadiliko mapya ya uongozi itawezekana kuwa bora zaidi iwapo watu wote watakubali kushirikiana katika kuwaongoza vijana katika maadili yaliyo sahihi.

"Tuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu Subhana Wataala, aibariki nchi yetu na awawafikishe viongozi wetu hasa Rais wetu na Makamu wake wa rais, Mawaziri, Manaibu na wote walioteuliwa katika nchi yetu wawe na ikhlas na uadilifu", alisema Katibu huyo.

Aidha alisema huu ni wakati muafaka wa kutubia dhambi kwa kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kuomba maghafira na kumtaka msamaha.

Waislamu wa Zanzibar wataungana na waislamu kote duniani ambao wanaadhimisha kuingia kwa mwaka mpya wa kiislamu ambapo Zanzibar wanakusudia kufanya maandamano ya amani Kumshukuru Mwenyezi Mungu.

No comments:

Post a Comment