Saturday, 11 December 2010

UNYANYASAJI WAFANYAKAZI MAJUMBANI WALAANIWA.

Unyanyasaji wafanyakazi majumbani walaaniwa

Na Sharifa Maulid
Jumapili 12 Disemba 2010


SERIKALI inatambua uwepo wa wafanyakazi wa majumbani ndio maana imetoa toleo maalum linalozingatia kiwango cha kima chao cha mishahara yao.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Ali Khamis Juma, alisema hayo alipokuwa akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya wafanyakazi wa majumbani Duniani.

Alisema kutokana na hali hiyo jambo linalotakiwa kuzingatiwa ni ufuatiliaji wa kazi zao ikiwemo masharti muhimu ya utendaji kazi.

Juma alisema mbali na watu kufanyakazi majumbani lakini bado kuna baadhi ya waajiri hawathamini, hawawapatii haki zao kwa kuwapa mikataba badala yake hutumia uwezo wao kuwadhalilisha.

Naibu huyo aliwataka waajiri nchini kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa kutoa haki anazostahili mfanyakazi sambamba na wafanyakazi wenyewe kujenga msingi mzuri wa kazi za staha.

"Serikali inaungana na shirika la Kazi Duniani (ILO) na kuona umuhimu wa kuandaa mikataba wa kuweko kazi za staha kwa wafanyakazi majumbani", alieleza Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alifahamisha kuwa, katika mkataba huo mambo mbali mbali yamezingatiwa ikiwemo kupata mishahara, likizo, mapumziko, mikataba ya kazi na faragha.

Aidha aliwataka wafanyakazi majumbani kujiunga katika jumuiya yao ili kuwa na sauti moja na kueleza yale yote ambayo watafanyiwa kinyume na maadili ya kazi.

Mapema akitoa salamu za shirikisho la Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Suleiman Omar, alisema wafanyakazi wa majumbani wanachangia maendeleo kwa waajiri na familia zao, hivyo ni vizuri waajiri kujitahidi kuwapatia haki zao na kuwathamini kama binaadamu.

Alisema wafanyakazi hao wanapewa majukumu makubwa katika nyumba na kuyatekeleza bila kujali saa anazofanyakazi na aina ya kazi anazozifanya.

Kongamano hilo limezungumzia juu ya Mkataba wa ILO ya wafanyakazi wa majumbani pamoja na umuhimu wa wafanyakazi majumbani kujiunga na jumuiya yao ya ZATHOCODAWU.

Wakati huo huo akilifunga kongamano hilo Katibu Mkuu wa ZATHOCODAWU, Ali Salum Ali alisema utekelezaji wa sheria za kazi umekuwa mgumu hivi sasa kutokana na sheria za kazi ambazo zimefanyiwa marekebisho 2005 kutokuwa na kanuni zake.

Alisema kesi nyingi zinazuhusu wafanyakazi na waajiri zinashindwa kufunguliwa na kuendeshwa vilivyo kutokana na kasoro hizo pamoja na Bodi ya kiwango cha mishahara kutokutana miaka minne sasa, jambo ambalo linasikitisha wafanyakazi wa majumbani.

Ujumbe wa mwaka huu 'Tufanyekazi za majumbani kuwa ni kazi ya Staha', kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Eacrotanal mjini hapa.

No comments:

Post a Comment