Friday, 3 December 2010

KITI CHA UMEYA ZANZIBAR KIMOTO.

Kiti cha Umeya Zanzibar kimoto


Na Mwantanga Ame


Ijumaa, 3 Disemba 2010


KIBARUA kizito kinamkabili aliyekuwa Meya wa Mji wa Zanzibar, Mahboub Juma Issa ambaye anatetea kiti hicho huku upinzani mkali ukimkabili kutoka kwa Diwani aliyejitokeza kukinyatia kiti hicho cha ubosi Manispaa.

Mahboub atalazimika kufanyakazi ya ziada kuitetea nafasi yake hiyo kwani mpinzani wake ni Diwani wa Wadi ya Miembeni, Abdurahman Khatib wote wakitoka kwenye jimbo moja la uchaguzi la Kikwajuni.

Mbali ya kinyang'anyiro cha kuwania Umeya kufikia patamu katika katika Mji wa Zanzibar, pia shughuli pevu imehamia katika Halmashauri za wilaya huku wagombea wakipigana vikumbo kuwania nafasi wa Uwenyekiti wa Halmashauri za Wilaya.

Uchaguzi wa Madiwani ulimalizika wiki iliopita baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa Wadi tisa za Unguja na Pemba kutokana na hitilafu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Tangu kumalizika kwa chaguzi hizo tayari baadhi ya vyama vilivyoibuka kupata wagombea wa kuchaguliwa katika majimbo na uteuzi wa viti maalum vya wanawake, wameanza zoezi la kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya Umeya wa Mji wa Zanzibar na Wenyeviti wa Hamlashauri Wilaya.

Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharib, kupitia msemaji wake Maulid Issa, kilieleza kuwa CCM chini ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini Magharib Yussuf Moahammed, kimeshakaa na kupitisha majina ya wanaotarajia kugombea nafasi hizo.

Alisema wagombea wanaowania nafasi ya Umeya na Uenyekiti wa Halmashauri za Wilaya wameshachukua fomu hizo na majina yao yameshajadiliwa na chama hicho.

Akizungumzia juu ya Umeya wa Mji wa Zanzibar Issa alisema waliochukua fomu hadi sasa ni pamoja na Meya aliyemaliza muda wake Mahboub Juma Issa, wa wadi ya Kisimamajongoo ambaye atachuana na Khatib Abrahman, wa wadi ya Miembeni ambao wote wanatoka Jimbo la Kikwajuni.

Kwa upande wa Naibu Meya, alisema nafasi hizo tayari nazo zimepata wagombea watano waliojitokeza kuwania ambapo baada ya vikao vya Chama kwa ngazi ya Mkoa kukaa, kilipitisha majina matatu ambayo yamewekwa pembeni kusubiri uchaguzi wa Meya kukamilika.

Majina ambayo yanayosubiri baraka hizo Katibu huyo alisema ni la Diwani wa Wadi ya Mlandege, Khamis Mbarouk Khamis, Mussa Haji Idrisa wa Wadi ya Mwembemakumbi na Shara Ame Ahmed wa viti Maalum Wanawake.

Alifahamisha kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi la kupatikana Meya huyo majina hayo matatu yatafikishwa katika vikao vya Kamati maalum ya Chama kwa hatua ya awali ya kuwekewa alama na baadae kufikisha katika vikao vya Kamati Kuu ya CCM na Halmashauri Kuu ya Taifa kupata mgombea ataewania nafasi hiyo katika Baraza la Madiwani.

Aidha, Katibu huyo alisema uchaguzi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi, nao umeshafanyika na aliyepishwa kwa hatua za awali kuwania nafasi hiyo kwa Mwenyekiti ni Masoud Abrahman alieshika nafasi ya kwanza na Shaka Hamdu amekuwa wa pili na Omar Ali Khamis ni watatu.

Nafasi za Umakamu, Katibu huyo alisema watasubiri matokeo ya vikao ni pamoja na Amina Ali Mohammed, Aziza Abdalla na Msimu Seif.

Alisema kuwa vikao ambavyo vinatarajiwa kuyapitia majina hayo na kufanya uteuzi wake vinatarajiwa kukaa wakati wowote kuanzia wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment