Kipigo kimetupa ari kushinda leo-Stewart
Na Salum Vuai, Dar es Salaam
Ijumaa 3,Disemba 2010
WAKATI Zanzibar Heroes ikijiandaa kuimaliza michezo yake ya kundi B kwenye mashindano ya Chalenji kwa kuivaa Rwanda leo, kocha mkuu wa timu hiyo Stewart John Hall, amesema kipigo cha bao 1-0 mikononi mwa Ivory Coast, kimeamsha ari mpya ndani ya kambi yake.
Amesema pamoja na kufungwa juzi, lakini vijana wake wamedhihirisha uwezo mkubwa wa kupambana na kwamba bado wana nafasi ya kucheza robo fainali.
Muingereza huyo amefahamisha kuwa bado anaamini timu yake itaweza kupata matokeo mazuri leo na kujisafishia njia kutokana na soka la kuvutia waliloonesha wanandinga hao wakati wakiikabili Ivory Coast moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa kufika fainali ya ngarambe hizo.
“Tumefungwa kimchezo, lakini pia tumeonesha kuwa tunaweza kupigana na kila mmoja alifurahia mchezo wetu, ninachosema safari haijamalizika na kipigo hicho ndicho kitakachofungua mlango kwetu kucheza fainali”, alifafanua.
Alieleza kuwa kwa vile mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, hali hiyo ndiyo iliyoiangusha timu yake lakini anakusudia kufanya baadhi ya marekebisho kabla pambano la leo ili kuwapa raha Wazanzibari na Watanzania kwa jumla.
Nahodha msaidizi wa kikosi hicho Nadir Haroub ‘Cannavaro’, alieleza kuridhishwa na kiwango chao na jinsi mashabiki walivyoipokea timu hiyo na kuiunga mkono kwa kuishangiria bila kuchoka.
Hata hivyo alisema hawana wasiwasi kuwa timu hiyo itafika robo fainali, ingawa inapambana na timu ngumu ya Rwanda ambayo pia inahitaji ushindi kusonga mbele.
Baadhi ya mashabiki waliliambia gazeti hili kuwa Zanzibar Heroes ni timu yenye mwelekeo mzuri kwa siku zijazo na kuitaka kuongeza bidii kuhakikisha inafuzu kutinga fainali na mashindano hayo na hatimaye kutwaa ubingwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment