Maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania bara yafana
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Alhamisi 9 Disemba 2010
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, jana aliongoza Watanzania kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanzania bara.
Tanzania bara, iliyokuwa Jamhuri ya Tanganyika kabla ya Muungano wa mwaka 1964, ilijipatia Uhuru wake Disemba 9 mwaka 1961, ambapo hadi jana imetimia miaka 49.
Sherehe hizo zilizofanyika katika kiwanja cha Uhuru jijini Dar es Salaam, pia zilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Aidha pia zilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda, Spika wa Bunge Anne Makinda, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar, Mabalozi pamoja na viongozi waandamizi wa serikali za Tanzania.
Katika maadhimisho hayo ya siku ya Uhuru, Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama alikagua gwarige maalum lililoandaliwa na vikosi hivyo.
Aidha vikosi hivyo, vilipata nafasi ya kucheza gwaride huku vikipita mbele ya jukwaa kuu vikitoa salamu ya heshima na utii kwa mwendo wa pole na mwendo wa haraka.
Katika sherehe za jana pia zilinogeshwa na ndege za kivita za Jeshi la Wananchi wa Watanzania zilizokuwa kipita juu ya anga la uwanja wa Uhuru, pamoja na vikisoi vya jeshi hilo kupiga mizinga 21.
Mbali ya burudani hizo, sherehe za miaka 61, zilipambwa na vijana wa sarakasi ambao walionyesha sanaa za aina mbali mbali katikati ya kiwanja hicho, huku wanafunzi wa skuli ya kimatifa ya Hazina, wakionyesha ufundi wa sarakasi.
Maadhimisho hayo yalitumbuizwa na ngoma za aina tatu ikitangulia ile ya gonga kutoka Zanzibar, ngoma ya Sangula kutoka Ulanga, Morogoro na ngoma ya Lirandi kutoka Musoma, Mara.
Tanganyika ilijipatia uhuru wake mwaka 1961 kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza, kufuatia harakati za kudai uhuru zilizofanywa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Friday, 10 December 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment