Mkataba kusitisha machafuko maziwa makuu wasainiwa
Na Omar Said, Arusha
Alhamis,2 disemba 2010
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu, amesema kutiwa saini makubaliano ya kumalizwa kwa migogoro na vurugu katika Ukanda wa Maziwa Makuu unatokana na utashi wa dhati wa viongozi na wananchi wanaounda taasisi hiyo muhimu.
Alisema makubaliano yaliyofikiwa na kutiwa saini ya kumalizwa vurugu na migogoro katika ukanda huo unatokana na utashi wa dhati, ambapo amani na utulivu ndiyo tarajio la wananchi.
Balozi Mwapachu aliyasema hayo katika sherehe za utiaji saini usitishwaji na umalizwaji wa migogoro, vita na vurugu katika ukanda wa maziwa makuu ambapo mataifa kadhaa yakiwemo ya Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda.
Nchi nyingine ni pamoja na Angola, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) na Jamhuri ya watu wa Kongo, Afrika ya Kati, Sudan na Zambia, ambapo umoja huo wa ukanda wa maziwa makuu umejikita zaidi kuhakikisha kwamba kumaliza, kusitisha migogoro, vurugu, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na kuhamasisha amnai na utulivu miongoni mwa mataifa hayo.
"Umoja wa nchi unaounda maziwa makuu unajikita zaidi kuhamasisha amani, utulivu, maendeleo na kumaliza vita na migogoro miongoni mwa mataifa hayo, ni fursa ya wanajamii kujiendeleza kimaisha badala ya kukumbwa na hali isiyo ya utulivu", alisema Balozi Mwapachu.
Katibu huyo alisema kitendo cha kusainiwa makubaliano ya kumaliza migogoro na mapigano miongoni mwa mataifa hayo yanatoa fursa taasisi na jumuiya ya Afrika Mashariki kujishughulisha katika kuhamasisha mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria, UKIMWI na vitendo vya unyanyasaji katika jamii.
Aidha alisema makubaliano hayo yataweza kuchangia kuimarishwa kwa uchumi, maendeleo na utawala bora katika mataifa mbalimbali, kwani kabla ya kufikiwa hatua hiyo kulikuwa na tofauti sana miongoni mwao.
Naye Katibu Mtendaji wa Umoja wa Maziwa Makuu, Balozi Liberata Mulamula, alisema kazi kubwa iliyo mbele ni kuhakikisha kukuza na kuimarisdha dhana nzima ya utawala bora katika mataifa yanayounda umoja huo.
"Kazi kubwa ni kukuza na kuimarisha dhana nzima ya utawala bora, ambapo usalama na amani ni ajenda inayohitaji kuhimizwa miongoni mwa nchi wanachama, kwani kama hakuna utulivu na usalama ni vigumu kupata maendeleo"alisisitiza Balozi Mulamula.
Mkataba wa kuanzishwa Umoja wa Maziwa Makuu uliundwa huko Bujumbura, nchini Burundi, mwaka 2003 ambapo mataifa kadhaa yanahimiza kupiga vita, ugomvi na migogoro miongoni mwa mataifa hayo na kuimarisha demokrasi na utawala bora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment