Wednesday 1 December 2010

MAALIM SEIF : UCHAGUZI ULIKUWA SAFI, HAUNA GHILBA.

Maalim Seif: Uchaguzi ulikuwa safi, hauna ghilba







Na Abdi Shamnah, Pemba


Alhamisi 2, Disemba 2910

MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewathibitishia viongozi na wanachama wa chama cha CUF kuwa uchaguzi wa Zanzibar uliomalizika, ulikuwa safi na usio na ghilba.

Maalim Seif alisema hayo kwa nyakati tofauti, alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama hicho wa Wilaya za Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni kisiwani Pemba.

Alisema kutokana na hali hiyo na imani aliyonayo kwa Mwenyezi Mungu kuwa humpa yule amtakae, na kwamba hakujaaliwa malengo aliyonayo ya kuiongoza Serikali ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Umoja wa Kimataifa.

Maalim Seif alisema, Jeshi la Polisi, kwa mara ya kwanza katika uchaguzi, limefuata maadili ya kazi zake bila ya upendeleo, kinyume na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais, alisema ana imani na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuonyesha nia njema kwa kutekeleza vyema kivitendo matakwa ya katiba kwa kugawa kwa uwiano mzuri Wizara za Serikali yake.

Maalim Seif, aliwataka Wazanzibari kudumisha amani na mshikamano kwa kuweka mbele uzalendo wa utaifa na kuelezea imani yake ya kukua kwa maendeleo nchini kutokana na kuwepo kwa maridhiano.

Aidha aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CUF, kwenda katika Mabaraza hilo la kutunga sheria na kuwajibika ipasavyo ili kufikia lengo na matarajio ya wananchi.

Katibu huyo alliwaonya Wawakilishi hao kuwa yeyote atakaeshindwa kutoa hoja au kushindwa kuuliza maswali ya msingi katika vikao vitatu atalazimika kujieleza, pamoja na kuagiza kutumiwa taarifa zao Ofisini kwake.

Nae Makamo Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis, aliwataka viongozi hao kuhakikisha vijana wote wasio na vyeti vya kuzaliwa, wanaandaa utaratibu wa kuvipata, sambamba na kitambulisho cha Mzanzibari, ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2015.

Mapema katika salamu zao, Mawaziri waliotokea chama hicho walisema wanathamini sana dhamana walizokabidhiwa, hivyo watatumia uwezo wao wote katika kuwahudumia wananchi bila ubaguzi.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdillah Jihad Hassan, aliwathibitishia viongozi hao kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita, Sauti ya Tanzania Zanzibar na Televisheni ya Zanzibar, vitasikika na kuonekana kwa usahihi kisiwani humo, sambamba na gazeti la Zanzibar Leo kufika kwa wakati.

No comments:

Post a Comment