Monday 6 December 2010

UJENZI UKUTA WA UWANJA WA NDEGE WAANZA.

Ujenzi ukuta wa uwanja wa ndege waanza



Na Eva Msafiri, TSJ


Jumatatu 6 Disemba 2010

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeanza ujenzi wa ukuta utaozunguka Uwanja wa Kimataifa Abeid Amani Karume wenye urefu wa kilomita 12.

Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Idara ya Anga, Malik Mohamed Hanif, alisema ujenzi huo unafanyika chini ya Kampuni ya Sagea Satom ya Ufaransa, ambayo ndio iliyohusika katika upanuzi wa Njia ya kurukia ndege na kutulia hivi karibuni, ambapo tayari kazi hiyo imekamilika na kuruhusu ndege kubwa kutua nchini.

Alisema ujenzi wa ukuta utahusisha kilomita 10 utakuwa kwa kiwango cha zega na kilomita mbili utawekwa waya (senyenge) ili kuruhusu kuonekana vizuri kwa kiwanja hicho.

Alifahamisha kuwa, ujenzi huo unafadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni tano na kazi ya ujenzi wa zege imeshaanza na kufikia kilomita tatu katika maeneo ya Mombasa na Kisauni.

Aidha alisema maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa ya upanuzi wa njia ya kurukia ndege na kutulia, Zanzibar imepata sifa kubwa kutoka kwa kampuni mbali mbali zinazotoa usafiri ndani na nje ya nchi.

Malik alieleza upanuzi wa njia ya kurukia ndege na kutilia imefikia kwa urefu kilomita 3022 kutoka kilomita 2462 za zamani na kufikia upana wa kilomita 45 kwa sasa, jambo ambalo limeongeza uwanja huo kuwa na hadhi ya kimataifa.

Hata hivyo, alisema sambamba na upanuzi huo lakini barabara yake (njia ya kurukia ndege na kutulia), iko imara zaidi katika viwango vya kimataifa hadi kufikia PCN 61, ambayo inauwezo wa kuhimili vishindo vya ndege za aina mbali mbali.

Mkurugenzi huyo, alisema hivi sasa kuna maombi ya kampuni tatu za mashirika ya ndege, ambazo zimepeleka maombi ya kuja kuangalia uwanja huo ili kuweza kuleta ndege zao Zanzibar, ambapo miongoni mwa kampuni hizo ni Shirika la Oman Air na Kampuni Emirate.

No comments:

Post a Comment