Dawa ya unyanyasaji makazini yaja
Na Halima Abdalla
Jumapili 12 Disemba 2010
KAMISHNA wa Kazi kutoka Wizara ya Kazi na Uwezeshaji Kiuchumi, Iddi Ramadhan Mapuri, amesema wanaandaa ziara ya kufanya ukaguzi kwenye sehemu za kazi ili kuangalia matatizo yanayowakabili wafanyakazi.
Alisema ukaguzi huo utakaofanywa utasaidia kuweza kutatua migogoro ya kikazi watakayoibaini kwa wafanyakazi na waajiri.
Aidha Mapuri alisema, katika ukaguzi huo pia wataangalia mahusiano ya waajiri na wafanyakazi kwa kuangalia mikataba ya kazi, mazingira ya kazi, pamoja na masuala nyeti kama mishahara, haki na wajibu.
Sambamba na hayo alisema wanataka kujiimarisha ili kuweza kutoa takwimu zinazohusiana na ajira kwa wakati muafaka pamoja na kutelekeza sera ya ajira iliyopitishwa mwaka 2009.
“Lengo tunataka kamisheni ya kazi iwe na uwezo wa kufanya kazi kwa kujiimarisha zaidi na kwa nguvu zaidi ikiwemo kukamilisha kanuni za sheria za kazi ambazo hazijatayarishwa,’’alisema Mapuri.
Hata hivyo alisema katika kufanikisha hayo bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu ambao watakaofanikisha kufanya ukaguzi wa utatuzi wa migogoro hiyo ya wafanyakazi kwa kiwango cha ufanisi zaidi.
Sambamba na hayo alisema pamoja na changamoto zote zinazoikabili Idara yao karibu ya asilimia 75 ya migogoro wanayoipokea ya wafanya kazi wameweza kuitatua na kubwa wametayarisha mpango mkakati wa miaka mitano.
Saturday, 11 December 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment