Tuesday, 7 December 2010

DK. SHEIN SERIKALI KUIIMARISHA SEKTA YA AFYA

Dk. Shein: Serikali kuiimarisha sekta ya afyaRajab Mkasaba


Jumanne 7 Disemba 2010


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imepania kuimarisha sekta ya afya visiwani hapa.

Dk. Shein alisema mbali ya mipango iliyopo pia Serikali imedhamiria kuipa hdahi kamili hospitali ya Mnazi Mmoja kuwa hospitali ya Rufaa.

Rais Shein, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi pamoja na watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ikiwa ni hatua yake ya kuzitembelea Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu mjini Zanzibar, kilihudhuriwa na Makamo wa Kwanza na Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.

Aidha Rais Shein, alisema kuwa pia Serikali itazipandisha daraja baadhi ya hospitali za Wilaya na Mikoa.

Rais Shein, alisema Serikali yake itahakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto zote zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na maslahi kwa wafanyakazi wake, vifaa na majengo ya hospitali na taasisi za Wizara hiyo.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza watendaji hao kuwa mashirikiano baina yao yanahitajika ili ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi uweze kupatikana.

Nao viongozi na watendaji wa Wizara ya Afya walimueleza mafanikio yaliofikiwa katika sekta hiyo pamoja na changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kueleza mikakati waliyoiweka katika kupambana na changamoto hizo.

Pamoja na hayo, watendaji hao wamemuahidi Dk. Shein kuwa wataendeleza mashirikiano ya pamoja katika kuimarisha sekta hiyo ya afya.

No comments:

Post a Comment