Friday, 10 December 2010

WENYE VVU SINGIDA WAHAMASISHANA KUACHA UTEGEMEZI.

Wenye VVU Singida wahamasishana kuacha utegemeziNa Jumbe Ismailly, Singida
Alhamisi 9 Disemba 2010

CHAMA cha watu wanaoishi na virus vya UKIMWI (SIPHA) Mkoani Singida kimewataka wanachama wake kujenga utamaduni wa kutokuwa tegemezi kwa wafadhili kwa kubuni na kuanzisha miradi ya kujiongezea vipato.

Mjumbe wa kamati ya tendaji wa chama hicho, Juliana Samweli, alisema hayo kwenye semina ya siku tano ya kuwajengea uwezo wanachama wa chama hicho, kutambua wajibu wao.

Alisema kwamba idadi kubwa ya wanachama wa SIPHA, bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwa na miradi yenye uhakika inayoweza kukidhi mahitaji yao ya kila siku na hivyo kuwafanya wawe tegemezi.

Alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo kumechangia pia wanachama hao kuanza kujinyanyapaa wenyewe, jambo linalochangia watu wengine pia kuwatenga katika shughuli mbali mbali za kijamii

“Changamoto tunazokumbana nazo katika asasi yetu ni kutokuwa na miradi yenye uhakika ya kuweza kukidhi mahitaji yetu ya kila siku, sisi wenyewe kama wadau tumekuwa na unyanyapaa watu wamekuwa hawatuelewi”, alisema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa SIPHA, Selemani Athumani alisema malengo ya mafunzo hayo kuwa ni kuwajengea uwezo wanachama wake ili waweze kufahamu wajibu wao na wapo katika chama hicho kwa malengo gani.

Mwenyekiti huyo alizitaja changamoto zinazoikabili asasi hiyo kuwa ni pamoja na wanachama kutojua wajibu wao katika shirika, uhaba wa raslimali fedha kutokana na shirika kuwa si la kibiashara.

CHAMA cha watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (SIPHA) Mkoani Singida kina wanachama 52, kiliomba shilingi milioni 5 kutoka The Foundation for Civil Society kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanachama wake.

No comments:

Post a Comment