Monday 6 December 2010

WAZIRI ABOUD ASISITIZA NIDHAMU, UPENDO KWA WAFANYAKAZI.

Waziri Aboud asisitiza nidhamu, upendo kwa wafanyakazi



Na Luluwa Salum, TSJ


Jumatatu 6 Disemba 2010

NIDHAMU, upendo na ushirikiano ndio muhimili ndivyo vitakavyowezesha kupatikana kwa ufanisi kwenye sehemu za kazi.

Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud, alisema hayo wakati alipotembelea Afisi za Wizara hiyo zilizopo Pemba na kuzungumza kwa mara ya kwanza na wafanyakazi wa Wizara hiyo tangu kushika wadhifa huo.

Aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa jukumu kubwa la Wizara ya Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, ni kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kuwatatulia shida zao zinazowakabili.

Alisema watakapofanya kazi zao kwa uadilifu kutawafanya wananchi wawe na imani na serikali yao na kuwataka kuwa makini katika matumizi ya fedha za umma, pamoja na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Aidha aliwataka watendaji wa juu kutokuwa na upendeleo katika suala la ajira pamoja na nafasi za masomo zinapopatikana kwani wafanyakazi wote wana haki sawa, na kusema kufanya hivyo kutawajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi.

Kwa wake Afisa Mdhamini wa Wizara hio Pemba, Amran Massoud, alimpongeza Waziri Aboud kwa kuona umuhimu wa kukutana nao na kuahidi kushirikiana nae ,na kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata sheria.

No comments:

Post a Comment