Monday 6 December 2010

WAISLAMU KUADHIMISHA MWAKA WAO MPYA KWA MAANDAMANO

Waislamu kuadhimisha mwaka wao mpya kwa maandamano



Na Issa Mohammed


Jumatatu 6 Disemba 2010

WAUMINI wa dini ya kiislamu wa Zanzibar wanatarajia kufanya matembezi maalum ya kusherehekea kuingia kwa mwaka mpya wa kiislamu 1432, unaotarajiwa kuanza Jumanne ijayo.

Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, alisema waislamu hao wakiwemo wanaume na wanawake watafanya matembezi hayo katika barabara mbali mbali za mjini Zanzibar.

Akizungumza na waislamu katika msikiti Mkuu wa Mushawwar uliopo Mwembeshauri, Soraga alisema matembezi hayo yataanza katika viwanja vya Kisonge Michenzani, yatapita katika barabara mbali mbali za mji wa Zanzibar.

Sheikh Soraga alifahamisha kuwa matembezi hayo yatakayokuwa ya aina yake kufanywa visiwani Zanzibar na kwamba yatapambwa kwa kasda kutoka vyuo mbali mbali vya kiislamu viliopo mjini hapa.

Alisema matembezi hayo yatafuatiwa na mhadhara utakaofanywa katika viwanja hivyo ukiwa na lengo la kuwakumbusha waislamu mambo mbali mbali wanayopaswa kuyafanya wakiwa hapa duniani.

Katibu wa Mufti aliwataka waumini wa dini ya kiislamu kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha matembezi hayo muhimu hasa katika wakati huu ambao Zanzibar inakusudia kurejesha hadhi yake ya kuwa kitovu cha Uislamu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na kati.

Hata hivyo sheikh Soraga hakusema mgeni rasmi katika matembezi hayo atakuwa ni kiongozi gani.

No comments:

Post a Comment