Wednesday, 1 December 2010

RUDINI MAJIMBONI MKATEKELEZE MLIYOWAAHIDI WANANCHI -- BALOZI IDDI

Rudini majimboni mkatekeleze mliyowaahadi wananchi- Balozi Iddi



Na Abdulla Ali

MJUMBE wa Kamati Kuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amewataka viongozi waliochaguliwa kurudi kwenye maeneo yao kwa ajili ya kutimiza ahadi walizoziweka wakati wa kampeni za uchaguzi na zile zilizomo kwenye ilani.

Balozi Iddi alisema hayo alipokuwa katika kikao cha Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kilichofanyika katika Ofisi ya Chama ya Mkoa huko Mahonda.

Alisema uchaguzi umekwisha, lakini wananchi bado wanakabiliwa na kero nyingi majimboni mwao, hivyo ni wajibu wa wabunge, wawakilishi na madiwani kurejea majimboni kwa kushirikiana na wananchi hao katika kuondoa kero zao.

Makamu huyo wa Rais, alisema hakuna haja ya kusubiri ila huu ni wakati wa kuimarisha Chama na kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015.

“Ni kweli ndio kwanza tumemaliza uchaguzi hivi karibuni, lakini katika suala la maandalizi ya uchaguzi miaka mitano ni muda mfupi sana,” alisema Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM , alisema maandalizi ya mapema ndio yatakayokiletea ushindi chama CCM, ambapo kwao ni jambo la lazima kama ilivyo katika katiba ya chama hicho.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Haji Juma Haji alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa ushindi wake na pia kwa kumteuwa Balozi Seif Ali Iddi kuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment