Dk. Shein: 'Diaspora' ni muhimu kwa maendeleo ya nchi
• Asema walioko nje wasaidie nchi au kuwekeza nyumbani
Na Mwantanga Ame
Ijumaa 3 Disemba 2010
IDARA ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Shughuli za Wazanzibari waliopo Nje ya Nchi inakabiliwa na kazi ya kuhakikisha wataalamu na Wazanzibari walioko nje wanaandaliwa mkakati wa kurudi nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kurejea nchini kwenye mkutano wa tatu wa Ushirikiano baina ya Afrika na Jumuiya ya Ulaya.
Dk. Shein alisema Wazanzibari walio nje nchi na kuondoka Zanzibar kwa sababu mbali mbali lazima waandaliwe mazingira ya kurejea nyumbani waje wawekeze kwa wale wenye uwezo sambamba na kushiriki katika kujenga uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuna wataalamu wengi wa Kitanzania wakiwemo Wazanzibari waliamua kuondoka nchini kutokana na sababu mbali mbali, hivyo Idara hiyo itakuwa na kazi ya kuhakikisha inaandaa mkakati wa kuhakikisha wanachangia uchumi wa Zanzibar ama kurudi nchini kwao au hata huko waliko kwa kuwekwa utaratibu muafaka.
Dk. Shein alisema suala la kurejea wataalamu wa Zanzibar linawezekana endapo wataandaliwa mazingira mazuri ya kufanyia kazi pamoja na miundombinu.
Aidha alisema mkakati mwengine ambao Idara hiyo inapaswa kuufanyia kazi ni suala la uhimizaji wa viwanda vidogo vidogo kutoka kwa wawekezaji wazalendo walioko nchi za nje.
Alisema kuwepo kwa hali hiyo kutasaidia uzalishaji wa bidhaa nchini sambamba na kupata soko la ajira kwa vijana waliopo nchini.
Alieleza kuwa mkakati utaowekwa sasa ni ule ambao utawawezesha Wazanzibari wenyewe kurudi kuijenga nchi yao kwa kutumia utaalamu wao na pia kuwa na fursa ya kuwekeza Zanzibar huku wakitumia nafasi hiyo kwa kutoa ushawishi utaowashirikisha wadau wengine katika mataifa waliopo.
"Idara ya Diaspora ina kazi kubwa ya kuandaa mkakati wa kuona ajira za viwanda zinakuwa hasa viwanda vidogo vidogo na kuwashawishi Wazanzibari waliopo nje waje wawekeze wao wenyewe, ama washirikiane na wawekezaji kuwekeza Zanzibar ama wao warudi nchini kujenga uchumi wao", alisema Dk. Shein.
Alisema uwekezaji huo utaweza kuifanya Zanzibar bidhaa zake kuingia kwenye masoko yakiwemo yale ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC, na ya Umoja wa Ulaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment