Friday 10 December 2010

KUPOROMOKA KWA MAADILI KWACHANGIA UDHALILISHAJI WA WATOTO.

Kuporomoka maadili kwachangia udhalilishwaji watoto

Na Mwanajuma Abdi
Jumamosi 11Disemba 2010

HUKU wimbi la udhalilishaji watoto likiendelea katika jamii, baadhi ya wazazi na walezi wanadaiwa kuwa na mchango mkubwa unaosababisha watoto wao wadhalilishwe na kubakwa.

Washiriki wa mkutano wa mwaka uliwakutanisha wadau mbali mbali, kupitia Mradi wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (WEZA) unaoendeshwa na shirika la CARE Tanzania na Jumuiya ya Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),walieleza hayo katika Ukumbi wa Elimu Mbadala Rahaleo mjini hapa.

Walisema baadhi ya wazazi wa kike na wa kiume wanahusika kwa njia moja ama nyengine katika kuharibiwa watoto, kutokana na kuwavisha nguo fupi na za kubana, sambamba na akinababa kuwageuza watoto wao kama ni sehemu ya wake zao kwa kufanyanao mapenzi.

Akichangia katika mjadala, Mwakilishi kutoka Umoja wa Watu wenye Ulemavu, Salma Haji Sadaat, alisema wakati wa Sikukuu wazazi huwapaka watoto hina na piko kama watu wazima pamoja na kuwasuka rasta, jambo ambalo huwa vichocheo kwa wabakaji.

Alisema mbali ya watoto hao kurebwa kwa piko na hina pia huvishwa nguo vifupi zenye kubana huku miili yao ikionekana wazi.

"Starehe zimeongezeka, tunawarembea watoto wetu sana ndio sababu ya kudhalilishwa watoto pamoja na kuongezeka mimba za utotoni",alisema.

Salma alipongeza hatua ya Serikali za Mkoa kuzuia madisco katika viwanja vya sikukuu na kueleza kuwa makakati huo uendelee ili kuwaepusha watoto na vishawishi.

Nae Asha Aboud kutoka Jumuiya ya Kuwawezesha Wanawake, aliwatupia lawama wanaume na kuwataka wasifanye kisingizio cha mavazi kwani kuna watoto wa kiume wengi wanaharibiwa ikiwa hata hawavai nguo fupi.

Alisema wakati umefika kwa jamii kubadilika na kuungana pamoja katika kupiga vita masuala mazima ya udhalilishaji wa watoto.

Nae Siajabu Suleiman kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, aliwashauri akina mama wawe macho na waume zao kwani baadhi yao wanajihusisha na uharibifu wa watoto wao kwa kuwabaka na kuwalawiti.

Akitoa majumuisho katika mkutano huo wa siku moja, Meneja wa Mradi wa WEZA, Rase Matovu alisema mradi huo wa miaka minne umeanza mwaka 2008 na unamalizika Disemba mwakani, hivyo alitoa wito kwa waliowezeshwa watumie mafunzo hayo kuiendeleza jamii.

Mapema akiwasilisha maelezo ya mradi huo, Afisa Muwezeshaji, Ismail Salum alisema lengo lake ni kuchangia kupunguza umasikini kwa wanawake wa Zanzibar katika kuinua kipato chao na kuwaondoshea vikwazo.

Alisema kesi 36 zimeripotowa za ndoa na mimba za mapema, sambamba unyanyasaji wa kijinsia kwa kutekelezwa na waume zao kesi 22 kati ya hizo 15 zilipatiwa ufumbuzi.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Haji Makungu Mgongo, aliupongeza mradi huo kwa kufanya kazi vizuri katika kuwashirikiana na wanavikundi vinavyowashirikisha wanawake na wanaume katika Wilaya zote nne katika kuwajengea uwezo katika suala zima la kukuza uchumi na kuondokana na umasikini nchini.

No comments:

Post a Comment