DK SHEIN AHUTUBIA MKUTANO WA VIONGOZI WA ULAYA, AFRIKA
Asema Tanzania imepiga hatua malengo ya Milenia
Mafanikio yaonekana kwenye elimu, malaria Ukimwi
Na Rajab Mkasaba, Libya
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, zimepata maendeleo makubwa katika kutimiza malengo ya Milenia.
Dk. Shein aliyasema hayo jana kwenye hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa Mashirikiano ya Kimaendeleo kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, unaoendeleo huko Tripoli, nchini Libya.
Katika maelezo yake. Dk.Shein alisema kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Tanzania imepata mafanikio katika kutimiza malengo ya Milenia ni pamoja na kwenye sekta ya elimu ya msingi, kupunguza vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kupambana na Malaria pamoja UKIMWI.
Rais Shein alisema hatua hiyo ya maendeleo iliyofikiwa na Tanzania inatokana na mashirikiano yaliyopo baina ya washirika wa Maendeleo ambao wameiunga mkono Tanzania ikiwemo Jumuiya ya Ulaya (EU).
Dk. Shein ambaye anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano huo, alimpongeza Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kwa kuingiza mada ya kilimo na chakula, mada ambazo zimeelimisha na kutoa muelekeo kwa Afrika.
Alisema kuwa licha ya mafanikio yaliopatikana pia, Tanzania inakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinahitajika kuchukuliwa hatua ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Dk. Shein alisema kutokana na tafiti mbali mbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa zimeonesha kuwa Afrika haitoweza kutimiza malengo yote ya Milenia yaliyowekwa na badala yake mashirikiano zaidi yanahitajika kwa pamoja.
Dk. Shein alisisitiza kuwa mkazo zaidi unahitajika kwa nchi za Afrika katika kuimarisha sekta ya afya, chakula, elimu jinsia pamoja na usimamizi mzuri juu ya watu wenye mahitaji maalum.
'Watoto watakwenda skuli vizuri na wananchi wataishi vizuri katika nchi zao bila ya kujali tofauti zao kijinsia, umasikini utatokomwezwa”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa suala zima la kilimo na chakula ni jambo muhimu sana katika nchi za Afrika kwa kutambua kuwa Uchumi wa Afrika unategemea sana kilimo.
Alisema kuwa Tanzania imeweza kutia saini Programu ya Maendeleo ya Kilimo kwa Afrika (CAADP) kwa kutambua umuhimu wake katika maendeleo ya Taifa katika sekta ya kilimo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa iwapo mafanikio zaidi yanahitajika kuna haja ya kuongezwa upatikanaji wa fedha na mashirikiano zaidi kutoka Mfuko wa Fedha wa Ulaya (EDF) na nyenginezo.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika kufikia malengo kwa nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa soko la pamoja.
Dk. Shein alimpongeza Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, kwa maandalizi mazuri ya mkutano huo wa tatu wa EU na AU ambao mkutano wa mwisho kama huo ulifanyika miaka mitatu iliyopita nchi Ureno
Mkutano huo unatarajiwa kumaliza leo ambapo mada mbali mbali zilizungumzwa na kutolewa michango na viongozi mbali mbali waliohudhuria katika mkutano huo ikiwemo suala la uhamiaji, nishati, kilimo, uchumi, uwekezaji,mazingira, ushirikiano wa kikanda, Malengo ya Milenia na nyenginezo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment