Tume ya Haki za Binaadamu yaizindua serikali
Yaitaka iwashughulikie wanaopindisha sheria
Na Mwanajuma Abdi
Alhamisi 9 Disemba 2010
TUME ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora imesema wakati umefika kwa Serikali kuchukua hatua kali dhidi yawanaopindisha sheria kwa makusudi, wala rushwa na wavivu wasiowajibika katika kesi za udhalilishaji wanawake na watoto.
Kamishna wa Tume hiyo, Zahor Khamis, alieleza hayo kwenye taarifa aliyoitoa kupitia vyombo vya habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu duniania, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Kemea, Komesha Ubaguzi'.
Alisema Zanzibar ikiwa inaadhimisha siku hiyo kwa kuweka kipau mbele mambo ya msingi kwa kuishauri Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaopindisha sheria kwa makusudi na wanaokula rushwa katika kuharibu ushahidi wa kesi za udhalilishaji wanawake na watoto.
Alieleza hali ya udhalilishaji wanawake na watoto imekuwa ikiongezeka ndani ya jamii na kuonekana kama ni hali ya kawaida au kufikiwa ufumbuzi kwa njia za mkato ikiwemo kuzisuluhisha kesi hizo.
Aidha aliwatupia lawama Polisi na Hospitali kwa kutoshughulikia matatizo hayo kwa wakati, sambamba na mlalamikiwa kutofikishwa katika vyombo vya sheria.
Alieleza na iwapo mlalamikiwa anapofikishwa katika vyombo vya sheria mahakama huchelewesha kesi, kuharibu ushahidi na kuwepo mazingira ya rushwa.
Kamishna Zahour alifahamisha kuwa, tatizo hilo ni pana, ambapo mbali ya uwajibikaji wa vyombo ya umma pia kumejitokeza kwa tatizo la wananchi kutojua haki zao katika masuala ya udhalilishaji na kutoa wito kwa Taasisi za Serikali na Jumuiya za kiraia kuendelea na juhudi za kuwaelimisha wananchi ili wazijue haki zao.
Kwa upande mwengine alisema wimbi la migogoro ya ardhi nalo limekuwa likiongezeka, ambapo hivi sasa limekuwa ni tatizo la jamii na kushauri kufanyiwa kazi kwa kufanyika utafiti wa kina na hatimae kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
"Tusiridhike kusema kuwa migogoro ya ardhi itatatuliwa na mahakama au kudhani kuwa sheria ya ardhi ni nzuri sana na hivyo migogoro inatokana na ukorofi wa baadhi ya watu, kwa sasa hili ni tatizo la jamii hivyo halina budi kufanyiwa kazi ya utafiti", alifafanua Zahour.
Akigusia maridhiano ya kisiasa, Kamishna huyo alisema hatua iliyofikiwa Zanzibar imesaidia kuweka nchi katika amani na utulivu na kudumisha mshikamano uliondosha siasa za chuki na za kubaguana.
Aliongeza kusema kwamba, hali hiyo haina budi kutunza na kukuzwa ili wananchi wasirudi walikotoka, hivyo vyama vya siasa vinawajibu wa kuwaelimisha wanachama wao katika kuyaenzi maridhiano hayo na kuachana na maneno na mambo ambayo yanaweza kuathiri.
Maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu Duniani inatokana na madhila na madhara yaliyotokana na vita vikuu vya pili vya Dunia mwaka 1946, sambamba na kukumbushana kutekeleza mkataba wa Kimataifa wa Haki za Binaadamu, ambapo Tanzania ikiwa ni mwanachama wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na kuridhia mkataba huo.
Friday, 10 December 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment