Friday, 3 December 2010

MAZRUI ATAKA HESHIMA YA ZSTC IREJESHWE.

Mazrui ataka heshima ya ZSTC irejeshweLuluwa Salum na Is-haq Mohammed

Ijumaa 3 Disemba 2010
WAFANYAKAZI wa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kisiwani Pemba, wametakiwa kufanya kazi kwa bidii kwa lengo la kuongeza uzalishaji ili kulipatia pato taifa na wafanyakazi wa shirika hilo.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo kwa nyakati tofauti katika ofisi zake za Mkoani na Wawi Chake Chake.

Alisema ZSTC ni Shirika ambalo limeipatia sifa kubwa Zanzibar katika mataifa mbali mbali duniani kutokana na biashara zake kuwa na ubora, hivyo umefika wakati kulirejeshea heshima shirika hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa.

Alisisitiza kuwa kufanyakazi kwa bidii na kwa uzalendo na kuondosha tofauti zao za kisiasa ndiko kutakakoiletea Zanzibar mabadiliko sambamba na kupiga hatua kimaendeleo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Thuwaiba Edington Kisasi, aliwataka wafanyakazi kuwa na mashirikiano kwani mashirikiano pekee ndiyo yatakayopelekea kuleta mabadiliko yaliyokusudiwa.

Nao wafanyakazi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko walimuomba Waziri Mazurui, kuyashughulikia matatizo yanayoikabili wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi kama vile magari, kurejeshwa majengo ya wizara hiyo yaliyochukuliwa na baadhi ya wafanyabiashara, na kuwezeshwa kwa kuimarishwa sekta ya viwanda na biashara.

Mazrui pamoja na ujumbe wake walitembelea maeneo tofauti yaliyo chini ya Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na maghala ya karafuu, majengo yaliyokuwa ya Bizanje, karakana za ZSTC, Kiwanda cha makonyo na viwanda vidogo vidogo vya kukaushia matunda na samaki.

No comments:

Post a Comment