Kikwete apigia debe kujitosheleza kwa chakula
Na Omar Said, Arusha
Ijumaa,3 Disemba 2010
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka viongozi wa Jumuiya hiyo kuhakikisha kwamba suala la usalama wa chakula na mabadiliko ya hali hewa yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Rais Kikwete alisema tatizo la usalama wa chakula na mabadiliko ya hali ya hewa ni mambo muhimu yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili uwepo uhakika wa chakula katika eneo hilo.
Kikwete, alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika ukumbi wa Ngurdoto, nje kidogo ya jiji la Arusha.
Alisema hatua ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili masuala ya usalama wa chakula na mabadiliko ya hali ya hewa hayana budi kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na haraka, ili kupunguza ama kuondosha kabisa athari hiyo kwenye ukanda huu.
"Usalama wa chakula na mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kuwashirikisha wananchi kwa kutumia kilimo bora chenye tija, umwagiliaji”, alisema Dk. Kikwete.
Aliwataka viongozi wa Jumuiya hiyo kuhakikisha suala la usalama wa chakula na mabadiliko ya hali ya hewa yanachukuliwa kwa uzito wa aina yake, ili kuweza kupatiwa majibu yanayoweza kutoa tija na ufumbuzi wa kudumu.
Aliongeza kuwa iwapo kutazalishwa chakula kilicho bora na safi kinaweza kuleta ushindani katika soko la kimataifa na kuwafanya wananchi wa ukanda huu kupata mafanikio yanayoweza kutokomeza athari ya umasikini.
Alizishauri nchi wanachama kutoa kila aina ya msaada na msukumo katika kuwapatia ufumbuzi wakulima wa ukanda huu, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye sekta hizo ambazo katika kilimo kina mchango mkubwa kwa mataifa hayo.
Alikumbusha kuwa uzalishaji na usambazaji wa chakula ni lazima utokane na ziada ya inayozalishwa katika sehemu mbalimbali za ukanda wa Afrika Mashariki, kwani uzoefu unaonesha kwamba baadhi ya maeneo kwenye ukanda huu kuuzwa chakula kinachotegemewa na badala yake husababisha athari miongoni mwa jamii.
"Tunahitaji kuweka mikakati makini na mahiri inayoweza kusaidia kusambaa kwa jamii mbalimbali kwenye mataifa yetu na kuwasaidia chakula kilicho na usalama ambacho kimetokana na ziada ya uzalishaji" alifahamisha Rais Kibaki.
Alizishauri nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuhamasisha wafanyabiashara wa mazao ya kilimo walime mazao yanayoweza kustahamili ushindani katika masoko mbalimbali na kujipatia faida inayohitajika kujikwamua na athari ya umasikini miongoni mwa watu wake.
Mkutano huo unatarajiwa kumalizika leo ambapo Rais Kikwete ataukabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Friday, 3 December 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment